Na MWANDISHI WETU
TAASISI ya Doris Mollel (DMF) inayohusika na afya ya watoto njiti imesema itaendelea kushirikiana na serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuongeza kasi ya kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati 'njiti' kuokoa maisha yao.
Pia, imeipongeza serikali kwa jitihada kubwa inazoendelea kuzifanya za kuhakikisha inaboresha mazingira ya kina mama wanaojifungua watoto njiti, ikiwemo kujenga wodi zao katika Hospitali mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa Dk. Sylvia Rambo, alipomwaakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Doris Mollel katika mafunzo ya uandishi wa habari yaliyofanyika jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mtoto njiti duniani.
"Hadi sasa tayari tumezifikia hospitali 85 nchi nzima katika kuchangia vifaa tiba ikiwemo mashine za kupumulia, vitanda vikiwa na thamani ya zaidi ya bilioni 1.5," amesema
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Watoto na Mjumbe wa Bodi ya taasisi hiyo, Albert Chota ameipongeza Taasisi hiyo ya Doris Mollel, kwa jitihada kubwa inazoendelea kuzifanya za kuokoa watoto njiti kwa kutoa vifaa tiba mbalimbali na kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari huku akiiomba serikali kuongeza idadi ya wahudumu wa afya, ambao wataisadia kuokoa maisha ya watoto njiti.