TARURA WILAYA YA KILOMBERO YAJIPANGA KUTEKELEZA MIRADI

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Kilombero, Mhandisi  Sadick Karume (kulia), akikagua barabara inayosimamiwa na TARURA wilayani humo.

NA Mwandishi Wetu, Kilombero

Kufuatia malalamiko ya baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, kusuasua kwa  kutokamilika miradi mingi ya barabara sasa umepatiwa mwarobaini.

Akizungumza Meneja wa  Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilayani humo, Mhandisi Sadick Karume, amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa.

Karume amesema anafahamu changamoto nyingi za barabara zilizopo katika wilaya hiyo, hivyo TARURA wanajitahidi kutekeleza miradi hiyo, ikamilike kama ilivyokusudiwa. 

Amesema sema hategemei yeye kuwa sehemu ya tatizo na kukwama kwa miradi hiyo, itakuwa kwenda tofauti na maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kuwaletea wananchi maendeleo.

'' Nimesikia baadhi ya malalamiko niko tayari kuyafanyia kazi na wakandarasi nimewaelekeza kilichobaki ni utekelezaji kwani wananchi wanahitaji huduma bora",  amesema Mhandisi Karume.

Karume amesema Kilombero wanahitaji kuiamini TARURA hivyo ana amini kilio chao chao  baadhi ya barabara kitafanyiwa kazi mapema. 

Aidha Karume ametoa wito kwa wakandarasi wote waliopewa kazi katika wilaya ya Kilombero, kufanyakazi kama walivyokubaliana katika mikataba 

Amesema TARURA Kilombero imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara kuona kazi za ujenzi wa barabara inavyoendelea.

Amewataka wananchi wanaotumia barabara za Namawala kuelekea Mofu kutokuwa na wasiwasi kwani TARURA imesikia kilio chao 

Pia Karume amewataka wananchi hususan wanaotumia vyombo vya usafiri katika barabara ambazo bado ziko katika ujenzi kuepuka kuharibu na kufanya wakandarasi kuwa na kazi ngumu ya kufanya.