WATU WAWILI MBARONI KWA TUHUMA ZA UNYANYASAJI WA KINGONO NA WIZI

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuwatongoza wanawake, wanawawekea dawa za kuwalewesha, kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji wa kingono, kuwapigapicha, kuwatishia kuwaua wakitoa siri za udhalilishaji huo na baadae kuwaibia simu, laptop na fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa kwa sababu za uchunguzi.

Muliro amesema watuhumiwa hao wamekamatwa na vitu mbalimbali walivyoiba, laptop 10, simu za mkononi 305, runinga 36, kamera 4, subwoofer 3 na makasha ya simu 160.

Amesema baadhi ya vitu vilivyokamatwa tayari vimetambuliwa na wamiliki na watuhumiwa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Vilevile watuhumiwa watatu wanashikiliwa na kuhojiwa kwa tuhuma za wizi wa vifaa vya boti, vikiwemo injini mbili aina ya YAMAHA 200P, betri mbili za boti zenye thamani ya milioni 160,307,200 na gari yenye za namba za usajili T485 CWU aina ya Suzuki, mali ya mfanyabiashara Teusin Van Bauren, raia wa Afrika Kusini.

Muliro amewataja watuhumiwa hao ni mkazi wa Vikindu, Msabaha Michael 'Askofu', Juma Athumani 'Dito' (Mbagala), Joseph Januari (Tandale Kwatumbo).

Wakati huo huo, Muliro amesema kuelekea sikukuu ya Chrismass na Mwaka mpya Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha wananchi wanasherekea kwa amani na usalama umeimarishwa  katika maeneo yote.

Amesema Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam inaendelea

kusimamia mifumo ya kuzuia, kubaini na kupambana na vitendo vya kihalifu katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, akionyesha vitu mbalimbali vilivyokamtwa kutoka wahalifu baada ya Jeshi la Polisi kufanya operesheni ya kukamata wahalifu, jijini Dar es Salaam. 

Vitu mbalimbali vilivyokamatwa kutoka wahalifu, jijini Dar es Salaam.