Na Hemed Munga, Ludewa
Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo sekta ya maji wametakiwa kufanya kazi kwa ufanisi, ubora, kukamilisha kwa wakati na kuzingatia thamani ya fedha.
Wito huo, umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe,Victoria Mwanziva, alipofanya ziara ya kimkakati ya kukagua wa miradi ya maji wilayani humo, mkoani Njombe.
Amesema kupitia mradi huo utakapokamilika, wananchi watapata huduma ya majisafi na salama yatakayowatosheleza katika matumizi yao.
Victoria amesema kazi kubwa inayofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya maji wilayani humo, kuhakikisha wananchi wanapata huduma maji ya uhakika kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani.
"Ndugu zangu wananchi hakika tunamshukuru Rais Dk. Samia kwa sababu ametuletea Wanaludewa fedha Sh. bilioni 13.866, ambazo zimetekeleza miradi saba ya maji ambayo itaongeza huduma ya upatikanaji maji kutoka asilimia 74.3 hadi 79.7, vijijini na asilimia 100 kwa wakazi wa mji wa Ludewa", amesema.
Pia, Victoria amewataka wataalamu wa ngazi zote kuendelea kuielimisha jamii kutunza vyanzo vya maji na miundombinu kwa lengo la kunufaisha vizazi vijavyo.
Victoria ameongozana na viongozi mbalimbali wilayani humo, katika ziara hiyo Kata ya Mavanga, Ludewa, Iwela, na Manda kukagua hali ya upatikanaji wa maji na hali za miradi inayotekelezwa.