AIR FRANCE KUSAIDIA WENYE UHITAJI

 


Na MWANDISHI WETU

Shirika la Ndege la Air France, linatarajia kufanya harambee kukusanya fedha za kuwasaidia watu wenye uhitaji nchini.

Harambee hiyo inatarajiwa kufanyika mwaka huu ikiwa ni mipango ya shirika hilo kuhakikisha wanarudisha kwa jamii walichokipata.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Air France KLM kwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini, Nigeria, na Ghana Marius van der Ham, amesema malengo yao kwa mwaka huu ni kufanya harambee hiyo kuhakikisha wanachangisha fedha za kusaidia jamii kwa watu wenye uhitaji.

 “Tumejiwekea malengo mbalimbali mwaka huu ikiwemo kufanya harambee ambayo tutakusanya fedha kwa ajili ya kusiadia watu wenye uhitaji katika maeneo mbalimbali,” alisema.

 Amesema pia wanaendelea kuboresha huduma zao za usafiri wa anga barani Afrika kuhakikisha abiria wao wanaendelea kufurahia safari katika nchi mbalimbali.

Amesema Air France itaendelea kutoa huduma ya usafiri wa anga katika nchi mbalimbali na kuwahakikishia abiria usalama mkubwa wa usafiri kutokana na teknolojia ya kisasa wanayoitumia.

 “Tutaendelea kuboresha huduma zetu ziendelee kuwa za kisasa ikiwemo kuwahakikishia abiria usalama wa viwango vya juu.

 “Abiria wa Air France wanaosafiri kwa ndege kutoka na kuingia Afrika, wataendelea kufurahia huduma zetu kwa kila safari ambapo tunawahakikisha usalama wao na mizigo,” alisema.