KATIBU WA UVCCM WILAYA YA IRAMBA, AWATAKA VIJANA KUJITOLEA KATIKA SHUGHULI ZA KIJAMII



Na HEMEDI MUNGA Iramba,

Katibu wa Umoja wa  Vijana wa CCM Wilaya ya Iramba, Aman Daudi, ameunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kupanda miti katika Shule ya Msingi Kibululu, Kata ya Ntwike, mkoani Singida, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 47 ya CCM.

Daudi amesema wamepanda miti 200 ya matunda na miale katika shule hiyo kwa lengo la kutunza mazingira na kuhakikisha vijana wanashiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Amesema vijana wanatakiwa kujitolea katika shughuli mbalimbali kwa sababu anayejitolea popote alipo chama kinamuona.

Kwa upande  wa mwanachama wa CCM, Ramadhani  Magola, amewasihi vijana kuendeleza tabia ya kuwa na nidhamu na kujitolea kwa ajili ya Chama wakati wowote na kwa hali yoyote.

"Niwaombe vijana wangu nidhamu itawapeleka mbali, nidhamu ndio msingi wa chama chetu, tangu kuzaliwa mwaka 1977, kimebeba watu wengi, hivyo nanyinyi msikosekane," amesema.

Aidha, amewataka vijana hao kutokukata tamaa, hivyo wawe na ari hususan kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuhakikisha CCM inapata ushindi wa asilimia 100 na uchaguzi mkuu wa 2025.