WAZAZI NA WALEZI WATAKIWA KULEA WATOTO WAO KATIKA MAADILI NA UADILIFU WAWE VIONGOZI BORA


Na HEMEDI MUNGA Iramba, 

Katibu CCM Mkoa wa Singida, Lucy Shee, amewataka Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Kata ya Old Kiomboi na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama wilayani Iramba, kuwalea watoto wao kimaadili na uadilifu kwa sababu viongozi bora wanatoka katika familia iliyolelewa vizuri.

Lucy amesema hayo katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe hao, wazazi na walezi ndiyo wenye jukumu la kulea watoto wao vizuri ili waje kuwa viongozi bora katika kuwatumikia wananchi.

Amesema viongozi hao wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa tabia njema kutokana na vitendo na kauli zao za uaminifu.

Lucy amesema viongozi hao wanatakiwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia wajibu, kwa haki na mipaka yao.

Pia, amesema wawe na tabia ya kukubali kujifunza kwa watu wadogo kwa sababu huenda anajua zaidi na mdogo kujifunza kwa mkubwa huenda akawa anafahamu zaidi yake.

"Lazima tukubali kujifunza wakati wote na tujifunze bila ya kikomo," amesema.

Naye Katibu Mwenezi wa CCM wa mkoa huo, Elphas Lwanji, amewataka viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa katiba na miongozo iliyowekwa na Chama hicho.

Amesema viongozi hao kuendelea kuhakikisha uhai wa Chama kwa kuingiza wanachama wapya ambao wamesajiliwa kwa mfumo wa kielektroniki.

Lwanji amewasisitiza viongozi kufanya vikao vya kikanuni, kusikiliza kero na kutaja mafanikio yaliotekelezwa kupitia Ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2020 hadi 2025.

"Ndugu zangu, Old Kiomboi ni moja ya kata ambayo mmeletewa miradi mingi na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, hivyo kuweni mstari wa mbele kupigia debe yaliotekelezwa na Rais wetu," amesema. 

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda, amewakumbusha falsafa ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya kuwataka viongozi kutenda yale watu wanaowaongoza wanategemea kuyaona kwa  viongozi wa 
Chama hicho.

Mwenda amesema viongozi hao wana wajibu wa kuendelea kutunza heshima ya CCM na kutoonekana katika maeneo ambayo yanadaiwa kutokua ya  maadili kwa viongozi.

" Niwahusie kuziishi imani za Chama cha Mapindunzi kwa sababu kinaheshima kubwa ndani ya nchi, Afrika na duniani", amesema.

"Na sisi wengine hatukotayari kuona heshima ya chama chetu inavurugwa kwa sababu yako wewe, tutakua wakali, kulinda chama chetu, hadhi na heshima ya viongozi," amesema.

Naye Katibu Mwenezi wa tawi la Meli katani hapa, Elieze Msolomon amewapongeza viongozi hao kwa sababu ya tabia ya kukumbushana mara kwa mara, hivyo wanafahamu kinachokuja mbele yao na kuahidi kufanya kazi ipasavyo.

Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Lucy Shee, akizungumza na wajumbe wa Halmashauri kuu ya Kata ya Old kiomboi na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Iramba, katika  semina elekezi, wilayani humo. (Picha na Hemedi Munga)