PUMA ENERGY YAWATAKA WATANZANIA KUDUMISHA AMANI, UPENDO NA UMOJA

Watanzania wametakiwa kudumisha umoja, amani na kumuunga mkono Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza majukumu yake pamoja kuliombea taifa.

Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Puma Energy, Dk. Selemani Majige, wakati wa futari iliyoandaliwa na kampuni hiyo kwa wateja na wadau mbalimbali, jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.

Amesema katika kipindi hichi cha mfungo wa Ramadhan  na Kwaresima, wananchi waendelee kudumisha amani ili  uchumi uendelee kuimarika na biashara ziendelee vizuri, kwani kulinda amani ni jambo kubwa na endapo kutakosekana amani hata biashara haziwezi kufanyika vizuri.

"Kupitia mwezi mtukufu wa Ramadhan ni vizuri tuendelee kumuomba Mungu na kuendelea kumuombea Rais Dk. Samia aendelee kutuongoza na kudumisha amani katika taifa letu", amesema.

Pia, Majige amewaomba wananchi kuendelea kutumia mafuta ya kampuni hiyo na bidhaa zao kutokana na kuwa ubora na viwango vya hali ya juu.

"Tunawaomba muendelee kutumia mafuta ya Puma ili tuongeze faida na tukiongeza faida serikali inapata gawio na inapotoa gawio zinapatikana fedha ambazo zinakwenda kuhudumia jamii katika miradi mbalimbali", amesema.

Kwa upande wa Mwakilishi wa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Sheikh wa Wilaya ya Temeke, Sheikh Zailai  Mkoyogole, amesema katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan, jambo zuri ni kuzidisha wema kwani wanadamu ni wakosaji mbele za Mwenyezi Mungu.

Mkoyogole amesema katika mwezi huu mtukufu wajitahidi kuyafuata mafundisho ya Uislamu kwa kuonyesha upendo na matendo ya huruma, pia wasaidie wale wenye uhitaji na kudumisha umoja miongoni mwa jamii.

 "Ningependa kuwapongeza Puma Energy Tanzania kwa shughuli zao za kijamii, pia nawaasa muendelee na miradi hii ili kuzinufaisha jamii zenye uhitaji zaidi, pia binadamu tunamkosea Mwenyezi Mungu kwa vitu vingi hivyo sasa ameleta Mwezi mtukufu wa Ramadhan, kutubu kwa ambayo ameyafanya, kinachotakiwa katika mwezi huu ni kufanya mambo mema na kurejea kwake", amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, pamoja na kuwashukuru wadau waliojitokeza katika Ifutari hiyo, amewaomba wananchi kuwaunga mkono kwa kununua bidhaa za mbalimbali za kampuni hiyo, yakiwemo mafuta.

 Fatma amesema serikali inafanya jitihada za makusudi kuhamasisha matumizi ya gesi asilia ya kupikia, ambapo Puma Energy inajivunia kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhamia katika matumizi ya gesi asili ikiwa ni suluhisho la kupikia wa Watanzania.

Amesema jitihada hizo za serikali zitaleta mabadiliko makubwa ya kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa na kupambana na mabadiliko ya tabianchi, pia gesi asilia ya kupikia hupunguza uchafuzi wa mazingira katika makazi ya wananchi. 

"Puma Energy Tanzania tunatambua mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia, katika suala la nishati safi hivyo tutaendelea kusaidia kwa lengo la kuhakikisha mazingira yanalindwa na matumizi ya nishati safi kwa watanzania yanakuwa kipaumbele", amesema.