KISHKI ATANGAZA OFA KUGHARAMIA NDOA 100 BURE

Na MWANDISHI WETU, Dar es Salaam

Taasisi ya Al Hikma Foundation imetangaza neema ya kugharamia  ndoa 100 kwa vijana wa kitanzania huku ikitangaza vigezo 10 kwa watakao hitaji kufunga ndoa hizo. 

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Nurdeen Kishki, amesema huo ni mwendelezo wa taasisi hiyo kurejesha shukrani kwa watanzania baada ya kumalizika kwa  mashindano makubwa ya 24 ya kuhufadhi Qur'an tukufu Afrika yaliyofanyika Machi  24 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Amesema mwaka jana Al Hikma Foundation ilijitolea kufungusha ndoa 70 kwa vijana na mwaka huu vijana 100 wa kiislamu watanufaika na ndoa hizo.

"Katika kuliendea jambo hili tuna mashariti na vigezo ambavyo mhusika atatakiwa kuvitekeleza,"alisema sheikh Kishki.

Ametaja vigezo hivyo kuwa mhusika lazima awe mwislamu, raia wa Tanzania, asiwe na mke, awe ameposa na kukubaliwa.

"Pia awe amejaza fomu maalumu ya maombi inayotolewa ofisi za Al Hikma Foundation, awe amefanya usahili baada ya kujaza fomu na kukubaliwa na awe tayari kufunga ndoa ya pamoja jijini  Dar es Salaam", amesema.

Kishki amesema kuwa vVigezo vingine ni mhusika awe amethibitishwa na imamu wa eneo lake, walii wake aridhie masharti hayo na awe na chanzo cha kujipatia riziki.

Aidha amesema dirisha la usajili wa ndoa hizo litafunguliwa Aprili 8, mwaka huu na kuwataka vijana wa kitanzania kujitoleza.