Na HEMEDI MUNGA
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amewaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu anaendelea kufanya makubwa yanayoboresha ustawi na kujali afya zao.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Urughu, wilayani Iramba mkoani Singida, Nchemba amesema Rais samia, anagusa maisha ya mtu mmoja mmoja nchini.
Amesema fedha zinazoletwa Iramba na maeneo mengine nchini zinakwenda kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo, vikiwemo vituo vya afya katika kila tarafa na maeneo muhimu nchini.
"Tuendelee kumuunga mkono Rais wetu, fedha anazotoa haziishii katika makaratasi ni vituo vya afya vinavyoonekana kwa macho, mtu anaejali afya yako amekutakia mema sana kwa sababu bila ya afya huwezi kufanya kazi," amesema.
Nchemba amesema mtu anaejali afya yako anakupa mtaji wa kufanya kazi kwa sababu anaweza kuwa na mipango mizuri ya kazi lakini asipokua na afya njema hawezi kuitekeleza mipango hiyo.
Amesema hatua hiyo, ndio tafsiri halisi ya Rais Dk. Samia kuwapenda watanzania maana vituo vya afya wanavyoviona humu vipo nchi nzima.
"Ndugu zangu ninawathibitisha kuwa nchi nzima katika kila makao makuu ya tarafa na eneo la kimkakati lisilokua tarafa kuna kituo cha afya chenye hadhi ya hospitali ya wilaya,"
"Mama ametafasiri kwa vitendo kauli ya kuwapenda Watanzania na anashughulikia tatizo la ugumu wa maisha kwa kupeleka miradi mikubwa ya umwagiliaji hata ngazi ya kijiji ambayo inatoa majawabu", amesema.
Amesema anaorodha ya matatizo na kutoa majawabu kivitendo kwa sababu nchi nzima kuna miradi ya umwagiliaji na miradi ya kufungua barabara ambapo itabadilisha maisha ya watanzania kutoka katika ugumu.
Kwa upande wa Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda, amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alihakikisha usalama wa chakula na kilimo kwa kuagiza yachaguliwe maeneo kwa lengo la kupanua na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji.
Mwenda amesema hatua hiyo, itawafanya wananchi walime wakati wote wa kiangazi na masika kwa sababu watakua wanauwezo wa kuhifadhi maji.
"Tunao mradi wa Masimba katika Bonde la Wembere ambapo tumeishaletewa zaidi ya sh bilioni 3 na kutenga hekari 36,000, ambazo zitaendelezwa kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji," amesema.
Aidha, amethibitisha kuwa tayari wataalamu, maofisa wa umwagiliaji watatu wameishafika kujitambulisha ofisini kwake ambao wanashirikiana na wenyeji na kazi tayari imeanza.