MWIGULU AHIMIZA WANANCHI KUENDELEA KUTUNZA MISITU


IRAMBA - SINGIDA

Waziri wa Fedha, pia ni Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Dk. Mwigulu Nchemba, amempongeza na kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyoendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ule wa bwawa la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwigulu ametoa pongezi hizo, wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kaselya, wilayani Iramba, mkoani Singida, ambapo vijiji vyote vimeishafikiwa na nishati ya umeme.

Amesema kuhusu suala la umeme hivi sasa siyo shida tena, hivyo serikali inaendelea kujipanga na kutekeleza kwa lengo la  kuhakikisha vitongoji vyote vinafikiwa na umeme maeneo yote nchi nzima.

Mwigulu amewataka wananchi kuendelea kutunza misitu kwa sababu wanaweza kupata fedha kufuatia mabadiliko ya kidunia, ambapo hivi sasa kuna watu wananua hewa ya ukaa.

Amesema  hivi sasa kuna baadhi ya vijiji  ambavyo vinadaiwa kuwepo nchini ikiwemo wilayani Tanganyika kuna watu waliotunza Misitu wanauza hewa ya ukaa inayotengenezwa kutokana na misitu.

Ameweka wazi kuwa  waliuza nishati hiyo  wakapata takribani sh bilioni nane ambazo zinawasaidia kujenga ofisi za kisasa, wanatengeneza madaraja ikiwemo mabweni.

"Ndugu zangu katika msitu huo, kinachovunwa hakionekani ni hewa tu, ukiwa na msitu umeshonana,  wataalamu hao  wanaupima na kutegesha mitambo yao huku wakivuna hewa ya ukaa ambayo wanaiuza," amesema Dk. Nchemba na kuongeza kuwa:

Sasa hiyo ni rahisi maana unatunza msitu halafu unauza hewa kitu ambacho hakimtoi mtu jasho ukilinganisha na kuchoma mkaa."

Kutokana na hali hiyo, Dk. Nchemba amesisitiza kuwa dunia imebadilika, hivyo eneo lolote linaloweza kuwa ni pori walitunze kweli kwa sababu ni hela hizo hivi sasa.

Mwigulu amesema teknolojia hiyo inasaidia wananchi kuvuna fedha, hivyo inakua ni msaada wa kutatua changamoto ndogo ndogo kuanzia ngazi ya kijiji au kitongoji.

Amesema kufuatia duniani kuwa na mabadiliko hayo, ikiwa wànavuna namna hiyo kila mwaka, waende wakatuze misitu kwa sababu sasa misitu ni biashara.

Pia, ameeleza biashara hiyo  haitaji kuwa ni misitu ya kupanda au kumwagilia inaweza kuwa miti ya kawaida tu iliyotengeneza kapori, hakika  itawasaidia kuuza hewa ya ukaa na kununua majiko ya gesi.

Kwa upande wa Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda, ameendelea kumshukuru na kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuijali wilaya hiyo kwa sababu aliipatia fedha za miradi ya maendeleo.

Mwenda amesema Rais Samia, amehakikisha kila kata ndani ya kata 20 za wilaya hiyo, ikipewa takribani sh  bilioni 2.4 ambazo zimekua zikijenga  na kutengeneza miradi ya maendeleo ambayo imetajwa kuwa mwarobaini wa changamoto zinazodaiwa kuwakabili wananchi katika sekta zote.

"Ndugu zangu niwaombe tuendelee  kumuunga mkono Rais wetu, hakika ametujali mno, haijawahi tokea tangu wilaya hii kuwa, shukran sana Rais wetu," amesisitiza.