Chatanda: Serikali imedhamiria kujenga vituo vya afya kila kata

Na MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda amesema serikali imedhamiria kujenga vituo vya afya kila kata, kwa lengo la kusogezakwa jamii hususan maeneo ya vijijini, ambapo huduma hizo bado changamoto. 

Chatanda alisema hayo wilayani Kwimba, mkoani Mwanza, jana alipokagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Akikagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Hungumalwa, Chatanda alifurahishwa na namna wananchi walivyojitolea kuchanga fedha za kununua eneo hilo wajenge kituo cha afya.

"Serikali imedhamiria kujenga vituo vya afya kila kata kwa lengo la kusogea huduma kwa jamii hususan maeneo ya vijijini ambapo huduma hizo bado ni changamoto, " alisema.

Aliongeza kuwa: "Serikali inafanya kazi kubwa kusogeza huduma za afya kwa jamii, hivyo wananchi wanatakiwa kuitunza na kuithamini miundombinu  hii".

Kituo hicho kinahudumia wakazi 23,798 wa Kata ya Hungumalwa ambao wameondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya baada ya serikali kutoa sh. milioni 500 zilizojenga  kituo hicho. 

Inaelezwa kituo kitahudumia vijiji vinne vya  Hungumalwa, Lunele, Buyogo na Mwang'ombe. Wananchi hao awalu walikiwa wakipata huduma afya katika Zahanati ya Kijiji cha Hungumalwa

Mkazi wa Hungumalwa, Asteri Masalu alisema waliamua kujitoa kwa moyo kuchanga fedha za kununua eneo hilo lililojengwa  kituo cha afya kwa lengo la kupata huduma za afya karibu.

Aidha, wananchi waliipongeza serikali kwa kutoa fedha za kujenga kituo hicho kitakachowasaidia kupata huduma muhimu za afya.

Mbali na serikali kutoa sh. milioni 500 kujenga kituo cha afya, wananchi  waliamua kuchanga sh. milioni 23.7 za kununua  eneo kilipojengwa kituo  hicho. Hadi hivyo, hadi hivi sasa fedha hizo za eneo zilizolipwa ni sh. milioni 16.5,  wananchi bado wanadaiwa sh. milioni nane kukamilisha malipo. 

Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Hungumalwa, Staniley Masawe alisema kituo hicho kitasaidia wakazi wa kata hiyo na za jirani kupata huduma muhimu za matibabu ambazo hapo awali walikuwa hawazipati.

Katika kuboresha huduma za afya  kituo hicho, Mbunge wa Kwimba Mansoul Shanif  alichangia sh. milioni mbili kununua samani  zinazotakiwa. 

Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kwimba, Sabana Salinja alisema ushirikishwaji wa wananchi katika suala la maendeleo  wilayani humo  linawasaidia kuelewa umuhimu  wa kuchangia maendeleo.