TPDC YAUNGA MKONO MPANGO WA NISHATI SAFI

Na MWANDISHI WETU

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio amesema ujenzi wa kituo mama cha kushindilia gesi asilia katika magari, eneo la Chuo Kikuu Dar es Salaam, ni sehemu ya mpango mkakati wa Serikali  inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Mpango mkakati huo umelenga kuhakikisha Watanzania wote wanatumia nishati safi katika  magari, kupikia na vyombo vingine vya moto.

Dk. Mataragio amesema hayo jana, alipotembelea eneo la ujenzi wa Mradi wa Kituo mama cha kujaza gesi asilia katika magari (CNG) , eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kituo hicho kinajengwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

‘’Serikali ina mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo tunategemea ndani ya miaka 10 kuanzia 2024-2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

"Serikali iko mstari wa mbele kuhakikisha usambazaji wa nishati safi unawafikia wananchi maeneo mbalimbali,’’ amesema.