UWT Dar wakemea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto



Na MWANDISHI WETU

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Dar es Salaam, Mwajabu Mbwambo, amekemea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyoendelea katika jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, jana, Mwajabu alisema matukio ya hivi karibuni yamezua taharuki na hofu katika jamii.

Amesema jamii inahitaji shughuli za kijamii kuendelea kwa kuhakikisha kuna ulinzi na usalama kwa watoto na jamii, kutokana na matukio hayo watoto wanakuiwa katika kipindi hatarishi.

"Ndugu waandishi wa habari hivi karibuni kuna matukio mawili yametokea yakiwemo kule Mbagala kwa mtoto wa miaka sita na tukio lingine la ukatili limetokea kwa mtoto wa kiume amekatwa shingo na msichana wa kazi, ndiyo maana UWT imeamua kuzungumza na jamii", amesema.

Mwajabu amesema Jeshi la Polisi linafanya kazi kubwa, hivyo amelitaka kufanya uchunguzi wa kina kubaini wahusika wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia mbaya.

Amesema ulinzi wa watoto ni jukumu la wazazi na jamii nzima, hususan wanawake ambao ndiyo wanakaa na watoto kwa muda mrefu.

Pia amezitaka wilaya zote tano kupitia UWT, Kata 102, matawi yake na kamati ndogo ndogo zinazoshughulika na ukatili wa kijinsia, asasi zisizo za serikali kuendelea kuelimisha jamii dhidi ya aina zote za ukatili wa kijinsia zinazofanyika ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine.

"Ukatili mara zote unaanzia katika ngazi za familia, kuna wakati mtoto amelawitiwa na mjomba, babu au shangazi lakini wanaficha na badala yake anayebaki na kovu la kisaikolojia ni mtoto aliyefanyiwa kitendo cha ukatili", alisema.

Mwajabu ameiomba jamii kuacha tabia ya kuzusha  taarifa zisizo na ukweli zinazopelekea taharuki  kwa wananchi kupitia mitanda ya kijamii na kusababisha taharuki kwa jamii.

Wakati huo huo, Mwajabu amewataka wanawake na jamii kujitokeza katika kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpigakura na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika mwaka huu wa uchaguzi wa serikali za mitaa.

"Niwatake wanawake wenzangu itakapofika muda wa uchaguzi tujitokeze kwa wingi twendeni tukagombee nafasi za uenyekiti wa serikali za mitaa", amesema.

Aidha Mwajabu amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji miradi mingi ya kimkakati, miradi ya maendeleo na kijamii inayogusa wanawake na Watanzania wote.

Amesema miradi inayowagusa wanawake moja kwa moja katika wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam ni uboreshaji wa vituo vya afya, ujenzi na ukarabati wa shule na miradi ya maji yenye dhana ya kumtua ndoo mama kichwani.