Ziara ya Balozi Dk. Nchimbi yafyeka ACT, CUF na CHADEMA Kusini

Ziara ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, inayoendelea katika Mkoa wa Mtwara na Lindi, imewahamisha viongozi waandamizi wa vyama vya ACT Wazalendo, CUF na Chadema walioamua kujiunga CCM.

Wakisindikizwa na mamia ya wanachama waliorejesha kadi zao za vyama vya zamani kwa kasi kubwa kwenye mkutano wa hadhara. 

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mpilipili, Lindi mjini, ukiwa ni mwendelezo wa ziara ya Balozi Nchimbi, amewapokea viongozi hao waandamizi wakiongozwa na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Lindi na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mchinga Ndugu Hamidu Bobali.

 Viongozi wengine mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Wanawake wa ACT Wazalendo Lindi Mjini, Hawa Kipara, Meneja Kampeni wa Wabunge ACT Wazalendo Lindi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana CUF Lindi Issa Sapanga, Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Pwani, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Mchinga, Mwenyekiti wa Wanawake Chadema Lindi Mjini pamoja na Wanachama 250 wa ACT Wazalendo, wote wamehamia CCM.

Wakati akikabidhi kadi yake ya ACT na kujiunga CCM, Bobali amesema nimeishi miaka 20 nje ya CCM ambako niliaminiwa katika ngazi tofauti ndani ya CUF na ACT Wazalendo hadi kuwa Waziri Kivuli wa Maji lakini nikiri niliyokuwa yanapigania Jemedari Samia ameyafanya kwa nguvu kubwa hivyo sina jinsi isipokuwa kujiunga CCM na kumuunga mkono. 

Amesema kule upande wa pili tulikokuwa ametupiga kwenye mshono, hakuna tena agenda. Sasa hakuna kingine zaidi ya kazi nzuri za Dkt Samiana wenzangu hawa sasa tupo tayari kumsaidia.

Naye Balozi Dk. Nchimbi akiwapokea wanachama hao wa vyama mbalimbali wakiongozwa na ACT Wazalendo amesema  “karibuni huku wanachama wote ni sawa na mtapata ushirikiano mkubwa sana kuanzia sasa na kikubwa mmesema mmerudi sababu ya mambo makubwa yaliyofanywa na Dkt Samia nawapongeza kwa kuliona hilo mapema sasa tukaifanye Lindi ya kijani.”