Tanzania yawanoa wataalamu wa Hali ya Hewa wa Afrika matumizi ya Rada

Na Mwandishi Wetu

 KATIKA kuwajengea uwezo wataalamu wa hali ya hewa kutoka Taasisi za Hali ya Hewa barani Afrika, Kitengo cha Elimu na Mafunzo cha Shirika la Hali ya Hewa Duniani kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kinachoendeshwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wameandaa mafunzo mahsusi ya matumizi ya data na taarifa za Rada za Hali ya Hewa. 

Mafunzo hayo yamefanyika  jijini Mwanza,Leo,  yakihusisha wataalamu wa Hali ya hewa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na wakiwemo viongozi wa TMA na Serikali.

Akifungua rasmi mafunzo hayo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa  Makame Mbarawa, ameeleza lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha zaidi uwezo wa wataalamu wa hali ya hewa kutoka baadhi ya nchi za Afika Mashariki na Kusini mwa Afrika katika matumizi bora ya taarifa za Rada za hali ya hewa kuboresha utabiri wa hali ya hewa na utoaji wa tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa kwa jamii.

Ameeleza, mafunzo hayo yanaendana na utekelezaji wa mpango ulioasisiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa utoaji wa Tahadhari kwa Wote (Early Warning for All EW4ALL) ifikapo mwishoni mwa mwaka 2027 na Sera ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ya ubadilishanaji wa data za hali ya hewa Kimataifa (WMO Unified Data Policy).

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Mwakilishi wa kudumu wa WMO, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a, alieleza, TMA imejiandaa vyema kupitia wataalamu wake katika kutoa mafunzo hayo.