Serikali yapokea gawio la sh.bilioni 4.35 kutoka TAZAMA

Na MWANDISHI

SERIKALI imepokea gawio la sh. bilioni 4.35 kutoka katika  uwekezaji wa Bomba la Mafuta la Tanzania hadi Zambia (TAZAMA), ikiwa ni rekodi kubwa ya ongezeko la gawio hilo kwa miaka mitano.

Matokeo hayo ya kutolewa kwa gawio hilo, kunatokana na utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuimarishwa na kuona tija ya uwekezaji huo aliyoyatoa katika ziara yake nchini Zambia.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam leo na Naibu Waziri Mkuu Dk. Doto Biteko, alipokuwa akipokea gawio hilo kutoka kwa viongozi wa TAZAMA hafla iliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Nifuraha kubwa leo, kuona matokeo chanya haya kwa vitendo na sio kwa maneno tu, hakika haya ni matokeo makubwa yaliyotokana na ziara ya Rais Dk. Samia alitembelea Zambia nakutoa maagizo ya kuboresha uwekezaji huu na utekelezaji wa maagizo hayo yaliyofanikisha matokeo haya ya leo,”amesema.

Akimkaribisha Dk. Biteko, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amempongeza Dk. Biteko kwa kupokea gawio hilo lenye tija kwa serikali, huku akisema ubia huo wa uwekezaji umekuwa na jita kwa ongezeko la kasi ikiwa ni hatua nzuri ya uwekezaji.