Na MWANDISHI WETU
MBUNGE Balozi Liberata Mulamula amesisitiza serikali kuweka mkazo zaidi sekta za viwanda na uwekezaji, hususan uwekezaji wa uchenjuaji( smelting) wa madini ili kufikia azma ya uchumi wa viwanda, kuwakomboa wananchi na Taifa kiuchumi.
Pia, amempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufungua nchi kupitia diplomasia ya uchumi, huku akiitaka serikali kuendelea kutenga bajeti kwaajili ya Balozi mbalimbali ziweze kutekeleza mipango yake.
Ameyasema hayo leo jijini Dodoma Bungeni, alipokuwa akichangia katika mpango wa maendeleo wa bejeti ya mwaka 2025/26, jijini Dodoma.
Amesema ni vyema serikali ikaongeza nguvu zaidi na kuwekeza fedha zaidi katika kipaumbele chake cha kukuza uchumi wa viwanda, hususan sekta ya madini huku akitolea mfano madini ya nickel yanayopatikana Mkoa wa Kagera na madini ya chuma na mawe yanayopatikana Liganga na Mchuchuma ambayo yakifanyiwa uwekezaji mkubwa yanaweza kukuza uchumi wa wananchi wa Mikoa hiyo na Taifa.
Ameipongeza Wizara kwa kuweka vipaumbele vyake vya kukuza uchumi, kuimarisha uzalishaji viwandani, utoaji huduma, na uwekezaji ambapo yakisimamiwa vizuri yatachochea ukuaji uchumi.
Vilevile, Balozi Mulamula alisisitiza umuhimu wa serikali kutenga bajeti ya kufanya tathmini na tafiti ya kipato na matumizi ya Kila kaya nchini na kuimarisha mfumo chanya wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na kuongeza nguvu kwa kuwa na sera mahsusi.