Miaka 63 ya Uhuru DC Mpogolo atangaza mikakati mitatu usafi wa mazingira



Na MWANDISHI WETU

 MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametangaza utekelezaji wa mikakati mitatu itakayo dumisha usafi katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

 Mikakati hiyo ni kufanyika kwa operesheni ya kuwapanga wafanyabiashara wadogo ‘machinga’ katika maeneo rasmi na kuwaondoa katika maeneo yaliyokatazwa.

 Aidha kuanzishwa kwa mashindano ya usafi katika masoko kila baada ya miezi mitatu na kuimarisha kampeni za upandaji miti na kufanya usafi katika fukwe za Bahari ya Hindi ili kutunza mazingira.

 Mpogolo aliyasema hayo Dar es Salaam, jana, katika maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika, ambapo aliwaongoza wananchi wa wilaya hiyo kufanya usafi katika masoko ya Ilala na Buguruni na kushiriki kampeni ya upandaji miti katika Ufukwe wa Dengu, Kata ya Kivukoni.

Mpogolo, alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuelekeza maadimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika kufanyika kwa shughuli za kijamii hususan usafi na upandaji miti.

Alisema, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ambayo ni sura ya Mkoa wa Dar es salaam ina mikakati mbalimbali ya usafi ambayo itatekelezwa kikamilifu.

Kuhusu kupanga machinga, Mpogolo alisema wapo ambao wameanza kurejea katika maeneo yaliyokatazwa.

Alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elhuruma Mabelya kufanya operesheni ya kuwaondoa na kuwarejesha katika maeneo yaliyoelekezwa.

“Mimi mwenyewe nitashiriki operesheni hii. Wamachinga warejee katika maeneo yao tuliyokubaliana. Tutawashirikisha wao. Siyo kila eneo Dar es Salaam mtu anatakiwa kupanga biashara,”alisema.

Mpogolo, aliitaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kuanzisha mkakati wa kushindanisha usafi katika masoko yote na soko litakaloibuka mshindi lipewe zawadi na cheti.

“Andaeni utaratibu huu ili tuimarishe usafi katika masoko yetu. Tafuteni majaji na vigezo vya masoko na zawadi,”alisema Mpogolo.

Alisema serikali inaendelea kujenga masoko ya kisasa wilayani humo ambapo miongoni mwa masoko yatakayojengwa ni Soko la Ilala.

Kuhusu upandaji miti, Mpogolo alisema Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, amekuwa akisitiza usafi wa mazingira na upandaji wa miti hivyo Wilaya ya Ilala itatekeleza kwa vitendo maelekezo hayo.

“Katika kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru tumepanda miti katika Ufukwe wa Dengu. Tutaendelea kupanda miti katika maeneo yetu mbalimbali. Dhamira ni kuitikia wito wa Makamu wa Rais Dk. Mpango na kuimarisha mikakati ya kulifanya jiji kuwa safi,”alisema.

Katika maadhimisho hayo, Mpogolo aliungana na wananchi, viongozi wa Jiji la Dar es Salaam, Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, wadau wa usafi , Umoja wa Waendesha Pikikipi Wilaya ya Ilala na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia Shirika lake la SUMA JKT.