MEYA WA JIJI DAR ES SALAAM, AMEZINDUA BOTI YA KUDHIBITI UVUVI HARAMU, SOKO LA KIMATAIFA LA SAMAKI FERI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

 Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, amewataka viongozi wa Soko la Kimataifa la Samaki Feri, kuhakikisha wanaitunza boti uokoaji waliyokabidhiwa.

Kumbilamoto alisema hayo wakati akikabidhi boti hiyo kwa lengo la boti hiyo ni kusimamia usalama na mazingira soko hilo katika Bahari ya Hindi.

Amesema boti hiyo lazima itumike katika malengo yaliokusudiwa na isitumike tofauti, lazima waisimamie kuhakikisha inafanyakazi muda wote itakapohitajika.

"Chombo hichi kikasaidie kudhibiti uvuvi haramu ambao hawana leseni, ili wakate leseni kuongeza mapato, pia watenge fedha za dharula kusiwepo na sababu ya kushindwa kufanyakazi boti hiyo kwa kisingizio cha kukosa mafuta", amesema.

Pia Kumbilamoto amempongeza Meneja wa Soko hilo, Denis Mrema, kusimamia makusanyo kuongezeka kutoka Sh. milioni 100 na kufikia Sh. zaidi ya milioni 150.

Naye Diwani wa Kata ya Kivukoni Sharik Choughule, amesema wakati anaomba kura ya kuchaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo, alitoa ahadi hiyo na kwamba ametekeleza Ilani ya CCM.

Pia Sharik amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya kuleta maendeleo kwa wananchi ikiwemo katika kata ya Kivukoni.

"Rais wetu Dk. Samia ameingia madarakani kwa muda mchache tu, lakini amefanya mambo mengi mazuri tena kwa haraka na anaendelea kuchapa kazi", amesema.