RAIS DKT. SAMIA KUSHUHUDIA UJAZAJI MAJI BWAWA LA JULIUS NYERERE, DESEMBA 22, 2022

Muonekano wa Tuta Kuu la kuzuia maji ya kufua umeme katika mradi wa Julius Nyerere (JNHPP), mkoani Pwani.


Muonekano wa sasa wa Handaki la kuchepusha maji ambalo litafungwa Desemba 22, 2022 ili kuanza zoezi la kujaza maji katika Bwawa la kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) mkoani Pwani.


Waziri wa Nishati, January Makamba (tatu kulia), akitoa maelekezo kwa ujumbe alioambatana nao, kuhusu kuanza kujaza maji katika Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP), litakalofanyika Desemba 22, 2022 mkoani Pwani. Katikati ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali.

Waziri wa Nishati, January Makamba (katikati), akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu kuanza kujaza maji katika Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere( JNHPP), litakalofanyika Desemba 22, 2022 mkoani Pwani. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande, akimueleza jambo, Waziri wa Nishati, January Makamba (kulia), kuhusu kuanza kujaza maji katika Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP), litakalofanyika Desemba 22, 2022 mkoani Pwani. Katikati ni Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Wizara Nishati , Mhandisi Innocent Luoga.

 

Na Zuena Msuya, Pwani

Waziri wa Nishati, January Makamba amewaeleza watanzania kuwa zoezi la kuanza kujaza maji katika Bwawa la kufua Umeme la Julius Nyerere (JHPP) litaanza tarehe 22 Desemba 2022 na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Watanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Makamba amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo Desemba 18, 2022 mkoani Pwani ambapo alisema kuwa hiyo ni hatua kubwa, Muhimu na ya kihistoria katika nchi yetu ya kutekeleza mradi huo.

Mradi huo kwa umefikia asilimia 78 ya utekelezaji wake tangu kuanza kwa mradi huo.

Alisema kuwa utokana na ukubwa wa zoezi hilo na umuhimu wa mradi huo kitaifa, ni ishara kuwa ndoto zetu za maendeleo ya Taifa katika kutekeleza mradi huo zinatimia kwa kuanza kujaza maji rasmi katika bwawa husika: Ambapo zoezi hilo litazinduliwa na kushuhudiwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Tunayo Faraja kubwa kwamba mjadala ambayo umekuwa ukiendelea kuhusu dhamira ya Serikali kukamilisha mradi huo angalau utaondoka sasa baada ya kufikia hatua hii, kwa sababu huu ni ushahidi tosha kwamba serikali, Rais, Wizara ya Nishati, na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tumefanya kazi kubwa ya kutekeleza mradi huu kwa nguvu, maarifa na juhudi kwa wakati wote, mahali tulipo fika sasa ni pa kujivunia, alisema Makamba.

Alifafanua kuwa Handaki la kuchepusha maji lina urefu wa mita mia saba (700), yaani viwanja saba vya mpira wa miguu na lilijengwa miaka mitatu iliyopita kwa gharama ya shilingi takribani Bilioni 235.

Licha ya mradi huu kuzalisha umeme, mradi mkubwa wa sekta ya Kilimo, Uvuvi, Usambazaji wa maji safi na pia mradi wa kudhibiti mafuriko ambapo baada ya kukamilika maeneo yaliopo bondeni yatawekewa utaratibu wa uzalishaji wa kilimo cha biashara.

Bwawa hilo pia litakuwa ni kivutio cha watalii kwakuwa liko ndani ya hifadhi na litabadili kabisa taswira ya hifadhi hiyo na thamani ya hifadhi hiyo itaongezeka ndani na nje ya Tanzania.

Vilevile ni mradi wa Miundombinu ya usafirishaji ambapo wakazi wa Mikoa ya kusini ikiwemo  Lindi na Mtwara wataweza kwenda Mikoa ya Dodoma, Iringa, Arusha na kwingineko kwa kupitia daraja kubwa kwa la pilli kwa ukubwa katika mto Rufiji bila kupitia Mkoa wa Dar es Salaam kama ilivyo sasa.

Serikali ya Misri ambao ni wakandarasi wake wanatekeleza mradi huo, watatuma ujumbe wa watu takribani mia tatu (300) ambao utakaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, pamoja vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mtendaji wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Maharage Chande aliweka wazi kuwa inakadiriwa kuwa misimu miwili ya kipindi cha mvua, itaweza kujaza maji katika bwawa hilo.

Tunaanza kujaza maji mwezi huu wa Desemba ambapo kuna mvua za vuli, pia tunategemea mvua za masika mwezi Machi 2023, ambazo zitakuwa mvua za msimu wa kwanza, pia tutapata vuli  ndani ya kipindi hicho, kisha tutapata zile za masika katika mwaka 2024  pamoja na vuli ya kipindi hicho, hivyo mvua mbili kubwa za masika zinaweza kujaza bwawa kwa hesabu zilizopo, Alisisitiza Chande.

zoezi hilo litahudhuriwa na watu takribani 2000 na litatangazwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari ili watanzania wote waweze kushuhudia maendeleo na hatua iliyofikiwa katika kutekeleza mradi huo.