FEISAL 'FEI TOTO ALIVYOTINGA TFF KUSIKILIZA MALALAMIKO YAKE DHIDI YA KLABU YA YANGA








 

Kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ametinga Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kusikiliza malalamiko yake dhidi ya klabu yake.

Yanga ilimshtaki kiungo huyo TFF kwa madai ya kuvunja mkataba bila kufuata utaratibu ambapo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, ilimuita Fei Toto kujibu malalamiko hayo.

Ilipofika saa 4.40 asubuhi, mwanasheria na meneja wa kiungo huyo na wale wa Yanga, wakiongozwa na Simon Patrick walikuwa katika Ofisi za TFF, wakisubiri kuanza kusikilizwa shauri hilo.

Mwanasheria wa Yanga, Wakili Simon na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andrew Mtine, waliwasili saa 3:40 asubuhi, waliwakuta wale wa Fei Toto, wakiwa wameingia nusu saa kabla.

Baada ya mahojiano ya dakika 40 mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Fei Toto na mawakili wake na wale wa Yanga walitoka kwa mapumziko kisha kutakiwa kurudi baada ya swala ya Ijumaa na chakula cha mchana.

Wakati wanaondoka katika ofisi za shirikisho hilo, Meneja wa Fei Toto ambaye ni baba yake mzazi, amesema bado hawajapata majibu wala hawajaona mwanga wowote kuhusu sakata hilo na kwamba hawezi kujua kama Fei Toto atarejea Yanga ama la na kusisitiza wanaojua hilo ni TFF.

Mkurugenzi wa Sheria na Masoko wa TFF, Boniphace Wambura, amesema shauri la Yanga na mchezaji huyo linaendelea kusikilizwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, likimaliza kamati itatoa ufafanuzi mbele ya wapenzi wa soka.

Desemba 24 mwaka jana, Fei Toto, aliandika barua ya kuvunja mkataba wake na Yanga kwa kuwapa kiasi cha sh. milioni 112, ambapo Yanga ilizikataa fedha hizo na kuzirudisha wakimtaka aheshimu mkataba.