NAIBU SPIKA ZUNGU AMEAHIDI KUYAFANYIA KAZI MAOMBI YA WANANCHI WA KATA YA MINAZI MIREFU

Naibu Spika Mussa Zungu (katikati), akipata maelezo kutoka kwa Diwani wa Kata ya Minazi Mirefu (kushoto), wakati alipokagua majengo ya SUDECO yanayomilikiwa na Wizara ya Kilimo, kuomba wapewe kwa matumizi ya kutoa huduma za kijamii katika kata hiyo, Dar es Salaam, jana. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Side.

Naibu Spika Mussa Azan Zungu (kushoto) na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Side na Diwani wa Kata ya Minazi Mirefu, wakiwa katika ziara ya kukagua majengo ya SUDECO na majengo ya TMA yaliyopo katika kata hiyo, ambayo yameomwa na wananchi yabadilishwe matumizi kuwa shule ya msingi na kituo cha Afya.

Baadhi ya majengo ya SUDECO yanayomilikiwa na Wizara ya Kilimo, ambayo wananchi wa Kata ya Minazi Mirefu, wameiomba serikali iwapatie yatumike katika shughuli za kijamii.



 NA MWANDISHI WETU

Naibu Spika Mussa Zungu, ameyapokea rasmi maombi ya wananchi wa Kata ya Minazi Mirefu ya kupewa majengo yaliyoachwa na serikali, tumike katika kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.

Zungu alipokea maombi hayo, baada ya kuyakagua majengo hayo ya SUDECO yanayomilikiwa na Wizara ya Kilimo na majengo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), katika kata hiyo, Dar es Salaam, jana.


"Haya ni majengo ya serikali na yametelekezwa kwa miaka mingi na nimepokea maombi yenu na nitahakikisha serikali itoe kauli kama bado inayahitaji kuyatumia au kuyarudisha halmashauri, halmashauri ijenge shule ya msingi na sekondari", alisema.

Zungu alisema serikali hii ni sikivu anaamini atasikiliz ombi yao na serikali italifanyia kazi na hatimaye wakafanikiwa kujenga shule na kituo cha afya katika kata hiyo ambayo haina shule ya msingi na kituo cha afya.

Pia Zungu alisema hivi karibuni kuna sheria mpya imepitishwa ya Bima ya Afya kwa wote, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan, ametaka iwafikie kila mwananchi.

"Endapo Bima ya Afya ikija na hakuna kituo cha afya, haitakuwa na faida, hivyo wananchi wapate bima za afya na viwepo hivyo vituo vya kutoa huduma za afya", alisema.

Naye Diwani wa Kata hiyo, Godlisten Malisa, alisema wameomba kupata shule ya msingi, sekondari na kituo cha afya katika majengo ya SUDECO yanayomilikiwa na Wizara ya Kilimo na majengo ya Mamlaka ya Hali Hewa (TMA), ambayo hayatumiwi kwa sasa.

Alisema tumemuomba Naibu Spika, Zungu kuwaongezea nguvu wananchi wa Kata ya Minazi Mirefu na Mbunge wa jimbo la Segerea, Bona Kamoli, kuhakikisha wanatekeleza Ilani ya CCM kwa kuwaletea wananchi shule na kituo cha afya.

Malisa alisema kata hiyo haina shule ya msingi na kituo cha afya, kwa hiyo endapo watayapata majengo hayo yatasaidia kuondoa changamoto ya wananchi kupata elimu na afya katika kata hiyo, ndiyo sababu kubwa kuyiomba serikali kuwapatia majengo hayo.