MAJALIWA AZITAKA HALMASHAURI KUSHIRIKISHA WACHIMBAJI UANDAAJI WA SHERIA NDOGO

Kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2022/2023 mchango wa sekta ya madini ni asilimia 9.6

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amezielekeza halmashauri zote za wilaya na miji, katika maeneo yenye madini ziandae sheria ndogo (by-laws) kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya madini ili ziendane na Sheria ya madini.

Ametoa agizo hilo, Mei 09, 2023, wakati akifungua Kongamano la Wachimbaji  Madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) katika ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza.

“Wakurugenzi wa Halmashauri wekeni mifumo bora ya kuweka tozo hizo na kuondoa kero kwa wachimbaji wadogo, punguzeni utitiri wa tozo kwa kubuni vyanzo vingine mapato”, amesema.

Amesema kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuweka mazingira bora katika sekta ya uchimbaji mdogo na tayari imeshaanza kufanya marekebisho ya baadhi ya Kanuni na Sheria ya Madini na kuboresha mazingira ya biashara.

“Lengo la kufanya haya yote ni kuwezesha wananchi hasa wachimbaji wadogo nchini na wadau mbalimbali kushiriki ipasavyo katika uchumi wa madini”, amesema.

Akizungumza kuhusu mchango wa Sekta ya madini kwenye pato la Taifa Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa umeongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017, hadi asilimia 7.2 mwaka 2021. 

“Pia katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2022/2023 mchango wa sekta ya madini ni asilimia 9.6”

Majaliwa amesema Serikali kupitia sekta ya madini imeweza kukusanya shilingi bilioni 409.66 sawa na asilimia 85.43 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 479.51 katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2022/2023.

Pia Majaliwa  ameiagiza Wizara ya madini kuharakisha mchakato wa kutafuta ufumbuzi wa suala Madini ya Lithium mapema iwezekanavyo ili kuweka wazi viwango vya uongezaji thamani kwa madini hayo kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Amesema kuwa Serikali imeendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kurasimisha maeneo yenye milipuko ya madini ambapo katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023 zimetolewa jumla ya leseni 6,381, zikiwemo leseni 3,865 za uchimbaji mdogo wa madini (PML), leseni 1,649 za biashara ndogo ya madini (Brokers).

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini ambapo hadi sasa jumla ya viwanda vitatu vya kusafisha wa dhahabu (Gold Refineries) vimeanzishwa viwanda vyote kwa pamoja vinauwezo wa kusafisha dhahabu kilogramu 515 kwa siku. Viwanda hivi vipo katika Mikoa ya Geita, Mwanza na Dodoma na vinafanya kazi”.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Madini,  Dkt. Stephen Kiruso, amesema kuwa Sekta ya madini ni nguzo ya maendeleo duniani kote “Sekta hii imesaidia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa na maendeleo ya mtu mmoja mmoja hapa nchini.

Amesema jitihada za kuikuza sekta ya wachimbaji wadogo, Serikali imetenga jumla ya maeneo 8 yenye ukubwa wa kilomita za mraba 112.29 kwenye mikoa ya Mwanza, Geita, Pwani na Shinyanga.

“Wizara ya madini itaendelea kusimamia sekta hii kwa weledi ili malengo ya Serikali yafikiwe”, amesema.

Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA). amempongeza Rais Dkt Samia Sukuhu Hassan katika kuhakikisha anaisimamia vyema sekta ya madini ili iweze kuketa tija kwa uchumi wa nchi, wachimbaji na watanzania kwa ujumla.

“Katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya sita upatikanani wa maeneo na utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini umeboresha, sisi wachimbaji wadogo mmetusikiliza, mmetusaidia mmetuheshimisha, alipo mama na wachimbaji tupo”, amesema.