Na Mwandishi Wetu
Waziri MKuu Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuzindua matembezi maalumu ya kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, yatakayofanyika nchi nzima.
Matembezi hayo yaliyoandaliwa na Bulding Natonal Consensus Foundation (BNC- Tujenge Mwafaka wa Kitaifa) ya hapa nchini yana lenga kumpongeza Rais Dk. Samia kwa utendaji wake, kuendeleza amani, umoja, mshikammano, mwafaka wa kitaifa na kuanzisha majadiliano ya katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa BMC, Abdallah Hamis, alisema matembezi hayo yatafanyika katika mikoa yote nchini.
“Tutangaza rasmi siku ya kuanza kufanyika kwa matembezi haya, mahari yatakapozinduliwa. Tunatarajia yatazinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,”amesema.
Amesema BNC imeamua kuja na matembezi hayo kutokana na utendaji uliotukuka wa Rais Dk. Samia, hasa kuleta utengamano katika taifa, kasi ya maendeleo ya kiuchumi na uongozi imara.
Hamis amesema matembezi hayo yanatarajiwa kupokelewa na Rais Dk. Samia.
Naye Katibu MKuu wa BNC, Ujamis Katanga, amesema taasisi hiyo ni changa lakini yenye maono ya kushiriana na jamii yote ya Tanzania bila kujali dini, ukabila, tofauti za kisiasa pamoja na kushirikiana na serikali kutangaza maendeleo.
Kwa upande wa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini, walipongeza Rais Dk. Samia, kwa kubuni miradi mipya, kuendeleza miradi iliyoanzishwa na watangulizi wake pamoja na kufungua fursa za kiuchumi kimataifa.
Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Angilikana Dayosisi ya Tabora, Dk. Isaya Mugaragu, amesema kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk. Samia, imevuta hata mataifa makubwa kutafuta fursa hapa nchini.
Mchungaji wa Kanisa la The Apostilic Ministry Tanzania, Baraka Chihamba, aliomba kuimarishwa kwa amani, mshikamano na utulivu.
Sheikh Abdulah Mohammed Said , Tasisi ya Wananyota, Kufundisha na Kuhifadhisha Quraan, alisisitiza Watanzania kulinda amani kwa gharama yoyote na kumpongeza Rais Dk. Samia kwa kusimamia misingi hiyo.