OFISI ZA SERIKALI SIYO VITUO VYA KUKUSANYIA MAPATO-DC MUNKUNDA

Na Shalua Mpanda-TMC Habari

Watendaji wa Serikali za Mitaa wilayani Temeke wenye tabia za kutumia madaraka yao kinyume na taratibu za utumishi wa Umma kuacha tabia hizo na kuwahudumia wananchi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mwanahamisi Munkunda, Juni 15,2023 wakati wa ziara ya kuzungumza na wananchi katika Kata ya Azimio.

Munkunda amewataka watendaji wa Serikali za Mitaa na watumishi wengine kutatua kero na changamoto kwa wananchi na kutambua nafasi walizo nazo wamezipata kwa lengo la kuwasaidia wananchi na sio kwa maslahi yao binafsi.

"Sikilizeni kero zao na kuzitatua,mnapata mishahara kwa kazi hiyo, haukufuatwa nyumbani kuombwa kufanya kazi hii.....na huduma katika Ofisi hizi ni bure msigeuze ofisi zenu kama vituo vya kukusanyia mapato".Alisisitiza mkuu wa wilaya.

Katika mkutano huo moja ya hoja iliyoibuliwa na wakazi wa kata hiyo ya Azimio ni suala la baadhi ya askari  wa ulinzi shirikishi kutokuwa waaminifu na kutokufuata taratibu za kazi ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Chang'ombe, Mrakibu wa Polisi Godfrey Mkangale, ameahidi kulitafutia  ufumbuzi wa haraka suala hilo.

Ziara hii ya mkuu wa wilaya ya Temeke ina lengo la kujitambulisha kwa wananchi pamoja na kusikiliza kero na changamoto mbalimbali katika maeneo yao.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mwanahamisi Mukunda (katikati), akisikiliza kero za wananchi katika Kata ya Azimio.