Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza mkakati kabambe wa kuhakiki fukwe ikiwa ni hatua ya kukomesha kushamiri kwa biashara halamu hususan magedo na magenge ya uhalifu
Ameyasema hayo Dar es Salaam, alipozindua kampeni ya usafi endelevu wa ufukwe wa Ununio, wilayani Kinondoni, iliyoandaliwa na Taasisi ya Women Impact Sustainable Enveronment Foundation (WISE) na kuhitimisha ziara yake wilayani humo.
Amesema moja ya mkakati ambao mkoa wa Dar es Salaam utatekeleza ni kuhakiki fukwe zote na kuangalia tija zake.
“Tunafukwe kutoka Pemba Mnazi Wilaya ya Kigamboni hadi mpaka wa Wilaya ya Kinondoni na Bagamoyo mkoani Pwani. Fukwe nyingi zimekuwa ni malango ya magendo mengi yanayotoka upande wa pili,”ameeleza Chalamila.
Chalamila amesema magendo hayo yanayoshamiri ni kutoka Zanzibar, Comoro na visiwa vya Anjuan.
“Fukwe hizi zimekuwa malango makubwa ya ukwepaji kodi ambayo Tanzania inngenufaika na fedha hizo katika miradi mikubwa ya maendeleo na yenye tija,” amebainisha mkuu wa mkoa.
Ameeleza imebainika fukwe nyingi mkoani humo zimegeuka kuwa vichaka na kimbilio kubwa la magenge ya uhalifu, hivyo mkakati huo unalenga pia kusambaratisha magenge hayo.
“Hatua hii ya tasisi ya Wise kuzindua kampeni endelevu ya usafi wa ufukwe wa Ununio ni muhimu wakati huu tunapoanza kutekeleza mkakati wetu huo,”amebainisha.
Pia Chalamila alisema moja ya mambo yaliyobainika ni kukithiri kwa uchafu wa chupa za vinywaji ambazo haziwezi kuchakatwa.
“Tutakaa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na watengenezaji wa bidhaa hizi. Watengeneze vifungashio vinavyo weza kuchakatwa.
Ikumbukwe hivi sasa tuko katika hatua za kubadili hata mfumo wa dampo letu la Pugu Kinyamwezi badala ya kulundika taka Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza taka hizo ziwe zinachakatwa upya,”ameeleza Chalamila.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amesema wilaya hiyo inafukwe zenye urefu wa kilomita 47, ambazo zingetumika vyema zingekuwa kivutio na uwekezaji mkubwa wenye tija.
“Ni maeneo ambayo ni utajiri mkubwa. Kama tutautumia vizuri kuendanna na ajenda ya Rais Dk. Samia ya Tanzania The Royal tour, tungekuwa na uwekezaji mkubwa hapa,”alisema Mtambule.
Awali MKurugenzi wa Taasisi ya Wise, Dorica Mwanji, amesema kampeni hiyo ya Ununio Sustainable Shores, ni endelevu na ina lenga kurejesha hadhi ya usukwe huo.
“Kampeni hii inaweeza kuleta athari chanya za mabadiliko ya tabia nchi. Sote tunajua shida ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo ni mafurik, ongezeko la joto duniani , ukame na mengine mengi,”amesema Dorica.
Dorica amesema Wise, itaendelea kufanya usafi katika ufukwe huo kuongeza uwekezaji, kipato cha wananchi na kukuza bishara.