Na Mwandishi Wetu
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inawashikilia na kuwahoji askari wa Kampuni ya ulinzi PASCO LTD 11, Maofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wawili na askari 6 kwa tuhuma za kujeruhiwa watu wawili ambao walipoteza maisha.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema suala hilo uchunguzi wake unaendelea kufanyika.
Muliro amesema Agosti 28, mwaka huu, saa nane usiku eneo la Kiluvya Ubungo, maofisa kutoka taasisi hizo wanadai wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, lilitokea kundi la watu wanaokadiriwa kuwa 30, wakiwa na pikipiki zilizokuwa zimebeba magunia ya mkaa ambayo ni mazao ya misitu na walipofika eneo la ukaguzi na kuamriwa wasimame.
Amesema watu hao walikaidi na kuanza kufanya fujo kubwa kwa kuwarushia mawe Maofisa wa maliasili na wenzao wakishinikiza pikipiki zilizo kuwa na mkaa kinyume na sheria ziachiwe.
Muliro amesema Maofisa wa timu hiyo waliokuwa na silaha walianza kufyatua risasi kwa lengo la kuwatawanya na kujilinda.
Amesema Hata hivyo ilibainika watu wawili walijeruhiwa katika purukushani hizo na walipoteza maisha baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Mloganzila.
Aidha Muliro amesema katika tukio hilo pikipiki 16 ambazo zilitelekezwa na watu hao na magunia ya mkaa vilipelekwa Mpingo House.
Amesema Polisi inachunguza mazingira yote ya tukio hilo kwa kushirikiana na mamlaka zingine za kisheria na halitasita kuwezesha kuchukuliwa kwa hatua zingine za kisheria kulingana na sheria za nchi.
Pia amesema watu waliokuwa katika kazi hiyo wako chini ya ulinzi na silaha zao zimepelekwa kwenye mamlaka za kiuchunguzi za silaha/bunduki, Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mloganzila kwa uchunguzi.