Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali itaendelea kuyaenzi mambo yote mazuri yaliyofanywa na marehemu, Bernad Membe, wakati wa utumishi wake Serikalini.
Membe ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje alifariki dunia Mei 12 mwaka huu katika hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Amesema marehemu Membe enzi za uhai wake alikuwa mwanadiplomasia mahiri kwenye medani za Kitaifa na Kimataifa, hivyo Serikali na Watanzania wataendelea kumkumbuka.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Agosti 26, 2023) aliposhiriki ibada ya kumbukumbu ya marehemu Membe iliyofanyika nyumbani kwa marehemu Rondo, Lindi.
Amesema weledi, nidhamu, uchapakazi na umahiri wa marehemu Membe uliitambulisha Tanzania katika medani za kimataifa na kutengeneza marafiki na mataifa mengine.
“Mheshimiwa Membe alikuwa na weledi wa kitaifa na kimataifa, jumuiya za kimataifa zinatambua umahiri wake na alijizolea sifa kwa sababu ya nidhamu na uchapakazi wake.”
Naye, Waziri wa Habari na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akizungumza kwa niaba ya familia ya marehemu aliishukuru Serikali kwa ushirikiano ilioutoa katika kipindi cha msiba.
“Namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukarabati wa kanisa ulioanzishwa na marehemu Membe".