BARRICK YAPONGEZWA KUUNGA MKONO JITIHADA ZA SERIKALI ZA KUBORESHA HUDUMA YA MAJI NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA KWA WANANCHI



NA MWANDISHI WETU


NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, ameipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuiunga mkono juhudi za Serikali kuboresha huduma ya maji, kutunza mazingira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.


Maryprisca alitoa pongezi hizo, mwishoni mwa wiki wakati alipokagua banda la kampuni hiyo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya 12 ya Siku ya Mara, katika uwanja wa Sokoine,  mjini Mugumu, wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara.


“Hongereni sana Barrick kwa shughuli mnazofanya kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na Serikali kwa ujumla katika uboreshaji wa huduma ya maji kwa wananchi, lakini pia utunzaji wa mazingira na kuinua uchumi wa nchi yetu,” alisema.


Pia Maryprisca amewataka Barrick North Mara kuendelea kuhakikisha shughuli zao za uchimbaji madini hazisababishi uchafuzi wa vyanzo vya maji na mazingira kwa jamii inayozunguka mgodi huo.


Kwa upande wa, Ofisa Mazingira wa Mgodi wa Barrick North Mara, Samwel Ingram,  alisema  shughuli za mgodi huo zinafanyika katika eneo lililopo ndani ya Bonde la Mto Mara, hivyo wanawajibika kulinda usalama wa vyanzo vya maji na mazingira yanayouzunguka.


Ingram alisema wanazingatia viwango vinavyokubalika kisheria katika kuchukua maji ya Mto Mara na kuyatibu kwa matumizi ya ndani ya mgodi na kuyasambaza kwa wananchi wa vijiji vinavyopakana nao.


 Pia alisema Barrick North Mara, inashirikiana na Serikali kupitia mamlaka husika zikiwemo Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijiji (RUWASA) na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) kuboresha huduma ya maji na utunzaji wa mazingira.


“Pia tunashiriki kwa vitendo kuiunga mkono Serikali katika juhudi za upandaji wa miti ili kutunza mazingira, sambamba na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji na mazingira,” alisema.


Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mara hufanyika Septemba 15 kila mwaka, ambapo nchi za Tanzania na Kenya zinazoshirikiana kuyaadhimisha hupokezana kuyaandaa kwa lengo la kuhamasisha uhifadhi na utunzaji endelevu wa Mto Mara ambao unatiririsha maji katika Ziwa Victoria.


Kauli mbiu ya Maadhimisho ya 12 ya Siku ya Mara mwaka huu wa 2023 inasema “Hifadhi Mto Mara kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi endelevu”.


Kampuni ya Barrick imeshiriki maadhimisho hayo kupitia Mgodi wake wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara.