NA MWANDISHI WETU, DAR
Wanawake nchini wameshauriwa kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa (SACCOS) kuepuka mikopo yenye riba kubwa ikiwemo ya kausha damu.
Pia, wametakiwa kuanzisha vikundi vya miradi ya ujasiriamali na kuungishana kwa kununua bidhaa wanazo zalisha hali itakayo wainua kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Mlezi wa Kata za Bunju na Makongo , wilayani Kinondoni, Diwani wa Viti Maalumu, Grace Mwashala, alipokuwa akikabidhi misaada kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kata ya Bunju, Dar es Salaam.
Diwani huyo amekabidhi vitenge, fedha taslimu , kadi za UWT na reja ambazo wanachama wa UWT Bunju watavutimia kuanzisha mradi .
Amesema vitenge hivyo ni kwaajili ya kukopeshana kisha fedha kuingizwa katika mfuko maalumu wa UWT wa Kata ambapo alitoa kiasi cha sh. 20,000 kufungua akaunti maalumu ya benki kwaajili ya miradi.
Grace amesema, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawake wanapata fursa za kiuchumi, hivyo ni muhimu kumuunga mkono kwa kuanzisha vikundi vya ujasiriamali na SACCOS.
“Anzisheni SACCOS ziwasaidie kujikwamua kiuchumi. Mnaweza wanawake. Acheni mikopo hii ya kausha damuna inayotoza riba kubwa,”ameeleza Diwani Grace.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, Fatuma Kange, alieleza umuhimu wa wanawake kuwa na SACOSS, zitakazo waepusha na mikopo yenye riba kubwa ya benki na kausha damu.
Kange ameeleza kuwa jicho la Rais Dk. Samia ni kuona wanawake wanainuka kiuchumi na ndiyo maana alianzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu ili kumwezesha mwanamke.
Aidha Kange, amewaasa wanawake kuungishana katika bidhaa wanazotengeneza na kuhakikisha zinakuwa na msimbo milia 'Bar Code' ili zikidhi viwango.