Na MWANDISHI WETU
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, limeridhia na kupitisha makadirio ya bajeti ya sh. bilioni 149.4. kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Akizungumza katika kikao cha baraza hilo, Meya wa Manispaa hiyo, Songoro Mnyonge, mesema bajeti hiyo imejikita kwa kiasi kikubwa katika miradi ya maendeleo na kutekeleza maelekezo ya serikali ya kujitegemea.
Meya Mnyonge, amesema, kiasi cha sh. bilioni 75.2 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu na sh. bilioni 74.2 ni mapato ya ndani ya halmashauri.
“Bajeti hii inathibitisha Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni inaendelea kujijengea uwezo wa kujitegemea. Hayo ndiyo malengo ya serikali kuzitaka halmashauri kujitegemea,”amesema.
Alibainisha, manispaa hiyo imekuwa mstari wa mbele kukusanya kodi hivyo bajeti yake kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu.
“Mapato ya ndani yamechangia kwa sh. bilioni 74.2 katika bajeti hii sawa na asilimia 49. Serikali kuu imechangia katika bajeti hii sh. bilioni 75.2 sawa na asilimia 50. Hivyo tofauti ni ndogo ya pato la ndani na ruzuku ya fedha kutoka serikali kuu,”amebainisha Meya Mnyonge.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Khanifa Suleiman, ameilishukuru baraza hilo kupitisha bajeti hiyo na kuomba ushirikiano zaidi kwa madiwani hao katika kuijenga halmashauri hiyo