NEEMA YAZIDI KUWASHUKIA WAKULIMA



Na MWANDISHI WETU, Dodoma

 NEEMA imezidi kuwashukia wakulima nchini, kufuatia Tigo na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), kuingia makubaliano ya mkataba, kuhakikisha wakulima wanapata huduma salama ikiwemo kuboresha mifumo ya mauzo ya mazao.

 Mkataba huo wa kimkakati, unaozingatia kanuni zote za serikali, unalenga kurahisisha na kuimarisha miamala ya kifedha kwa wakulima wanaopokea malipo ya mazao kupitia huduma ya Tigo Pesa.

 Akizungumza jijini Dodoma juzi, Mkuu wa Kitengo cha Tigo Pesa, Angelica Pesha, amesema makubaliano hayo mapya yanaashiria mwendelezo wa ushirikiano kati ya Tigo Pesa, TCDC na Chama cha Ushirika cha Wakulima ambapo malengo yake ni kuhakikisha wanaimarisha dhamira ya wakulima mbalimbali nchini.

 Amesema wamefikia makubaliano ya kutia saini mkataba mpya ambapo ule wa awali ulimalizika mwaka jana, lengo ni kuhakikisha wakulima wanafanya biashara za kuuza mazao kwa njia salama ya mtandao huo.

 Angelica amesisitiza huduma hiyo itaongeza uaminifu na usalama wa fedha za wakulima mbalimbali nchini.

 “Tumefikia makubaliano ya kuingia mkataba mpya kati yetu na TCDC na chama cha ushirika cha wakulima, lengo ni kuhakikisha wakulima wanaendelea kuuza mazao yao kwa uaminifu wa usalama wa fedha zao kote nchini,” alisema .

 Naye Mrajisi wa Chama Cha Ushirika na Mkurugenzi Mtendaji wa TCDC, Dk. Benson Ndiege, aliongeza: “Serikali kupitia TCDC ilikuwa inasubiri kwa hamu utekelezaji wa mkataba huu muhimu, kufanikisha kuleta mapinduzi ya miamala ya kifedha ndani ya sekta ya kilimo kupitia vyama vya ushirika katika kuwawezesha wakulima na kukuza uchumi wa nchi,”.

 Amesisitiza, hadi kufikia Januari mwaka huu, jumla fedha zilizochakatwa kwa mauzo ya mazao mbalimbali zilifika sh. bilioni 20 nchini.