DIWANI AMSHUKURU NA KUMPONGEZA RAIS DK. SAMIA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO KATA YA KIGAMBONI


Na Mwandishi Wetu

Kata ya Kigamboni, imepongeza na kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaletea fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya jamii na kuwaletea maendeleo wananchi

Akizungumza jana, katika sherehe ya maadhimisho ya Miaka 47 ya kuzaliwa CCM, Diwani wa Kata hiyo, Dotto Msawa, alisema fedha zilizotolewa na Dk. Samia, zimefanikisha kukamilisha miradi ya sekta ya afya, elimu, barabara na soko.

"Kigamboni tunamshukuru Rais Dk. Samia na kumuunga mkono katika uatawala wake, amefanya mambo mengi mazuri, katika kata yetu ameleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo ambayo baadhi imekamilika  na mingine inaendelea kutekelezwa", amesema.

Dotto amesema kwa upande wa sekta ya elimu, wanaendelea na ujenzi wa madarasa 16 katika Shule ya Sekondari Paul Makonda ambao umetumia Sh. milioni 950, pia ujenzi wa maabara, maktaba na ofisi za Waaalimu Sh. milioni 295. 

Amesema kata hiyo imetekeleza ujenzi wa vymba vya madarasa nne katika Shule ya Msingi Ufukoni kwa Sh. milioni 82, madarasa mawili  Shule ya Msingi Rahaleo kwa Sh. milioni 40, matundu 10 ya choo Shule ya Msingi Ufukoni Sh. milioni 13.8 na ukarabati wa madarasa sita ya Shule ya Msingi Kivukoni kwa Sh. milioni 13.3.

Kwa upande wa miundombinu ya barabara, Dotto amesema kata imetekeleza mradi wa barabara ya Chagani Polisi kwa Sh. milioni 894.2, barabara ya KKKT - Mikadi Sheraton kwa Sh. milioni 170.8 na Mikadi Sheraton kwa Sh. bilioni 2.1 kiwango  cha lami.

Pia amesema wametekeleza mradi wa ujenzi wa Mabweni katika eneo la Jumba la Mendeleo, Mtaa wa Kigamboni kwa Sh. milioni 200, ukarabati wa miundombinu ya choo na mifumo ya majitaka katika Soko la Feri kwa Sh. milioni 18.6, pamoja na kupokea Jenereta kubwa ya umeme katika Kituo cha Afya Kigamboni.

Dotto amesema katika kata hiyo kuna utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), ujenzi wa barabara za Mchava Njama, Majiposta, Urasa, Nguvu Kazi na Pikoli Polisi zote kwa kiwango cha lami na kuweka taa barabarani.