Na MWANDISHI WETU, Dar es Salaam
Kuzinduliwa kwa michuano ya Bonnah Segerea Cup 2024, kumeibua vuguvugu kwa viongozi wa Wilaya ya Ilala, kuunda timu ya soka itakayo sajiliwa kushiriki ligi mbalimbali hapa nchini.Akizindua michuano hiyo inayoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema kuna haja sasa kwa wilaya hiyo kuunda timu ya soka itakayo shiriki Ligi ya Championship na ikiwezekana Ligi Kuu Tanzania Bara.
" Wilaya ya Ilala ina majimbo matatu ambapo wabunge wake wamekuwa wakiandaa michuano. Kuna Bonnah Segerea Cup inayoandaliwa na Mbunge wa Segerea, kuna Zungu Cup inayoandaliwa na Mbunge wa Ilala na kuna Jerry Slaa inayoandaliwa na Mbunge wa Ukonga," amesema Mpogolo.
Amesema kupitia michuano hiyo ya majimbo inawezakana kuunda ligi itakayo husisha timu zitakazo ibuka mabingwa kisha kuundwa timu moja ya Wilaya ya Ilala.
Mpogolo amempongeza Bonnah kutokana na michuano hiyo kuwa chachu kubwa katika kukuza vipaji vya vijana huku akishauri elimu ya maadili kutolewa.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Side, amesema michuano hiyo inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kwa timu ya soka ya wilaya.
"Baada ya kumalizika michuano hii tunataka kuwe na mrejesho kwa washiriki na pia kuunda timu moja itakayo sajiliwa rasmi kushiri ligi mbalimbali.
Pia amesema kuna viwanja vya soka Segerea navyo ni Toto tundu Kecha na kuiomba serikali kuvijenga kwa mfumo wa kisasa.
Kwa upande wake Mbunge wa Segerea, Bonnah, amesema ameandaa mashindano hayo kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM hasa ikizingatiwa michezo ni ajira na ni afya.
"Timu 64 za soka zitashiriki. Jimbo la Segerea lina mitaa 61 hivyo kila mtaa utatoa timu moja," alisema Bonnah.
Pia amesema makundi ya waendesha bajaji, bodaboda, Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) kila kundi litatoa timu moja, amebainisha kuwa michuano hiyo itashirikisha timu za rede kwa wanawake katika mitaa yote.
"Mwaka huu mchezo wa rede utasimamiwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Ilala," amesema.
Bonnah amesema baada ya UWT kuratibu mchezo wa rede atawasilisha majina ya washindi.
Wakati huo huo, Bonnah amegawa jezi kwa timu zote zitakazoshiriki michuano hiyo.
Katibu wa Ofisi ya Mbunge wa jimbo hilo, Lutta Rucharaba, amesema michuano hiyo itafunguliwa rasmi Aprili 5 na kuhitimishwa Juni 2, mwaka huu, ambapo bingwa ataibuka na kitita cha sh.5,000,000, wa pili sh.3,000,000 na wa tatu sh.2,000,000.
Aidha kwa upande wa rede bingwa ataibuka na kitita cha sh. 2,000,000, wa pili sh.1,000,000 na watatu sh. 500,000.