Na Jeshi la Polisi Dar es Salaam
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama barabarani Tanzania DCP. Ramadhani Ng'anzi amesema tatizo la ajali za barabarani bado ni kubwa hivyo Jeshi la Polisi Kikosi cha usalama barabarani linafanya kila jitihada ili kuhakisha ajali zinatomezwa ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua madereva wasio tii sheria.
Kamanda Ng'anzi ameyasema hayo leo Julai 10, 2024 Jijjni Dar es salaam wakati akiwakabidhi vyeti na zawadi askari 5 wa kikosi hicho waliofanya kazi vizuri zaidi mwaka 2023/2024.
"Tunajua janga la ajali za barabarani hapa nchini bado ni kubwa na linatutesa lakini jitihada zinazofanyika, tunaamini ipo siku ile ndoto yetu ya Tanzania bila ajali kwa mwaka inawezekana" Alisema DCP Ng'anzi
Aidha ameongeza kuwa vyeti alivyowapatia ni ishara ya kutambua utendaji kazi wa askari hao ambao wamekua chachu kwa askari wengine.
Kwa upande wake Sajini wa Polisi, Asha Abdul wa kitengo cha elimu kwa Umma Polisi Kikosi cha Usalama barabarani Makao Makuu, ambaye amepata zawadi amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP. Camillus Wambura, Maofisa pamoja na viongozi wote kwa kutambua mchango wake ndani ya Jeshi la Polisi na kusema kuwa cheti hicho kimempa chachu na morali ya kuzidi kuongeza utendaji kazi.
Naye Sajini Meja wa Polisi, Rodney Msuya Mkuu wa nidhamu wa kikosi cha usalama barabarani Makao makuu amewaasa askari kuzingatia nidhamu katika sehemu ya kazi ili kutoa huduma bora kwa wananchi.