Hapi ampongeza Rais Dk. Samia kuibeba ajenda ya nishati safi

Na MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ally Hapi, amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa ya kuhamasisha ajenda ya nishati safi ndani na nje ya nchi, kuhakikisha Watanzania wanaondokana na nishati haribifu ambayo ina athari kubwa katika mazingira na afya.

Pia, amesisitiza Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Dk.Samia kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, ikiwemo ile ya kimkakati, hivyo wajipange kumpigia kura za kishindo mwakani katika Uchaguzi Mkuu.

Katibu Ally Hapi, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, alipokuwa akifungua kongamano la nishati safi, lililoandaliwa na Taasisi  isiyo ya kiserikali ya Acceleration of Life Skill Foundation (ALSF) kuhamasisha masuala ya nishati.

"Tunaendelea kumpongeza Rais Dk.Samia kwa kazi kubwa anayoifanya ndani na nje ya nchi, kuwa kinara wa nishati safi  na kutafuta fedha za kufanikisha nishati safi kwa wote hususan kwa wanawake walioko vijijini," amesema.

Ameeleza ajenda ya nishati safi kwa Rais Dk.Samia sio suala jipya anauzoefu nalo, kwani alianza nalo tangu akiwa Makamu wa Rais, ambapo aliifanya kazi kubwa ikiwemo kupanda miti na kuweka misingi mizuri ya nishati hiyo.

Akisoma risala  Mkurugenzi Thomas MChiwa  alisema wanaendelea kumuunga mkono Rais Dk.Samia katika, uhamasishaji wa nishati safi ambayo endelea nayo kwani inatija kubwa katika utunzaji wa mazingira

Amesema kuwa wanahamasisha katika upandaji wa miti kutunza mazingira huku wanaendelea kutoa elimu ya kuepuka ukataji miti kulinda na mazingira nchini.