Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Hamad awakumbusha wananchi kuwa Tanzania ni muumini wa kuhifadhi na kulinda haki za binadamu

IGUNGA - TABORA

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mohamed Khamis Hamad ameendelea kuwakumbusha viongozi mbalimbali na wananchi wilayani Igunga, mkoani Tabora kuwa Tanzania ni muumini wa kuhifadhi na kulinda haki za binadamu.

Hamad ameeleza hayo wakati wa semina ya mafunzo ya usambazaji wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi mbalimbali wakiwemo wale wa  dini, wakuu wa Taasisi, Idara, vitengo, madiwani, watendaji wa kata na vijiji katika ukumbi wa Maxwell wilayani  hapa.

"Ndugu zangu viongozi sisi hapa kwetu Tanzania kwa sababu ni waumini wa haki za binadamu tuliziweka kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kuziwekea mazingira na mifumo ya kuzisimamia," amesema.

Aidha, ameweka wazi  kuwa haki hizo  zinazo wajibu wake ikiwemo wajibu wa kushiriki kazi, wajibu wakutii sheria, wajibu wa kulinda mali za umma na wajibu wa ulinzi wa Taifa huku akihimiza viongozi kuendelea  kujitathimini kwa kiasi gani katika jamii zao  kwa kuanzia ngazi ya kitongoji,  kijiji, kata na kuendelea wanazingatia misingi ya utawala bora.