Mbunge Kilave amfagilia Rais Dk. Samia utekelezaji wa miradi ya maendeleo Temeke

Na MWANDISHI WETU

Mbunge wa Temeke, Dorothy Kilave, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na huduma za jamii katika kata 13 zilizopo wilaya hiyo ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.

Kilave amesema hayo, katika mkutano wa hadhara uliofanyika jimboni humo Kata ya Azimio, ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Amesema kazi kubwa imefanyika Jimbo la Temeke,  wanavyo vituo vya afya vitatu, zahanati kila kata na Hospitali ya Rufaa ya Temeke ambayo imejengwa vizuri na kuendelea kuboreshwa kwa ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.

Kuhusu elimu,  Kilave amesema shule zimejengwa za msingi na sekondari, ambapo wanafunzi wengi wameendelea kujitokeza kwa wingi kupata elimu.

Amesema wanaendelea kupata fedha za utekelezaji wa miradi ya elimu, kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora.

"Ni kata mbili tu za Makangarawe na Chang'ombe, ndizo pekee ambazo hazina shule za sekondari na suala hilo limeshafikishwa kwa Mkurugenzi na zitajengwa shule ya ghorofa," amesema.