Tanzania na China kushirikiana katika sanaa na utamaduni

Na MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk.Damas Ndumbaro, amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika sanaa na utamaduni kutimiza maono ya viongozi wa mataifa hayo ya kuimarisha diplomasia na kukuza uchumi.

Waziri Dk. Ndumbaro ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizindua Filamu maalumu ya 'Welcome To Milele' iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa timu ya madaktari wa China na Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano wa mataifa hayo na kutambulisha vivutio vya utalii na utamaduni.

"Filamu hii ni muhimu katika kuendeleza ushirikiano wa Tanzania na China, kwani inayoonyesha tamaduni zetu mbalimbali na kutangaza vivutio vyetu  vya utalii ikiwemo Mlima Kilimanjaro na hifadhi ya Serengeti.

"Filamu hii inaonyeshwa kupitia runinga ya Azam kwa tafsiri ya Kiswahili, hivyo itachochea ukuaji wa lugha ya Kiswahili kwa China ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wetu na China," amesema.

Ameeleza kuwa, filamu hiyo imebeba ujumbe mkubwa na kuonyesha ushirikiano wa kihistoria kati ya wananchi wa Tanzania na China, ulioasisiwa na viongozi waasisi wa mataifa hayo akiwemo Mwalimu Julius Nyerere.

Waziri Dk.Ndumbaro amesema uzinduzi wa filamu hiyo ni mwendelezo wa kuimarika ushirikiano wa Tanzania na China katika maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano tangu kuanza hivyo ni furaha kubwa kuona ukiimarika miaka kwa miaka.

Ameongeza, Filamu hiyo itaitangaza Tanzania kimataifa na kuonyesha vivutio vyake mbalimbali Kwa wachina na wananchi wengine.

Kwa upande wake, Balozi wa China NChini, Chen Mingjian aliipongeza serikali ya Tanzania chini ya Rais Dk.Samia  Suluhu Hassan kwa kuendeleza ushirikiano huo ambao umefika miaka 60 na kufanikisha filamu hiyo yenye mafunzo mengi ya tamaduni njema za mataifa hayo.