MAVUNDE AGEUKA MBOGO ATAKA MRADI WA DHAHABU MAGAMBAZI UANZE UZALISHAJI MKUBWA

Mgodi una wastani wa wakia 700,000

Na MWANDISHI WETU

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amebainisha kuwa kusuasua  kuanza kwa mradi wa uchimbaji dhahabu wa Magambazi uliopo Kijiji cha Nyasa Wilayani Handeni kunapelekea kuikosesha Serikali mapato na kuchelewesha maendeleo kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi huo.

Ameyasema hayo  leo Jijini Tanga alipokutana wawakilishi wa wananchi wa Handeni na Kampuni za CANACO Tanzania Ltd. na PPM Mining  ambazo zinahusika na utekelezaji wa mradi huo.

"Kwa mujibu wa taarifa za utafiti wa madini uliofanyika katika eneo la mradi huu, zinaonesha kuna zaidi ya wakia za dhahabu 700,000 na kwa hivi sasa mnasema mnazalisha dhahabu kiasi cha chini ya gramu 50, huku ni kuwanyima Watanzania haki ya kunufaika na rasilimali walizojaaliwa na Mwenyezi Mungu"

"Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza Wizara ya Madini kuhakikisha tunahamasisha na kuongeza shughuli za uchimbaji ili kuongeza mapato. Hivyo, ni dhahiri kwamba kunapokuwa na hali kama hii ya kusuasua kwa mradi ambao ulipaswa kuwa umefika mbali katika hatua za uwekezaji na uzalishaji, ni kurudisha nyuma jitihada za Serikali, na kwa kweli sisi tuliopewa dhamana hatuwezi kukubali.

Dhamira njema ya Serikali kwa wawekezaji ndiyo iliyotusukuma Wizara ya Madini kuunda Timu Maalum kwa ajili ya kufanya ukaguzi katika mradi huu ili ije itushauri namna bora ya kuufanya mradi huu kuanza uzalishaji kama tulivyokusudia.

Awali, akieleza umuhimu wa mradi huo kwa wananchi wa Handeni, Mbunge wa Jimbo la Handeni, Mheshimiwa Mhandisi John Sallu, ameishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za kutaka kuanza kwa mradi huo na kueleza matumaini makubwa ya wananchi wa Handeni kuwa tayari kupokea kuanza kwa uzalishaji katika mgodi huo wa dhahabu wa Magambazi.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Wakili msomi Mheshimiwa Albert Msando amekiri kukutana na wawekezaji hao mara kadhaa, na kuiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kuendelea kusimamia kuanza uzalishaji kwa mradi huo ili uchochee maendeleo ya wananchi wa Wilaya yake.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga,  Balozi Batilda Burhani  amebainisha kwamba pamoja na uwepo wa utajiri wa rasilimali nyingi katika Wilaya ya Handeni, bado wananchi wake wamekua wakiishi maisha duni na kusisitiza kuwa kuanza kwa miradi kama huo wa Magambazi kutakwenda kuchochea maendeleo ya Handeni na kuinua vipato vya wananchi.