TASAC, ZMA kuimarisha ushirikiano usimamizi wa usafiri majini nchini

Na MWANDISHI WETU

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), zimekubaliana maeneo zitakazoshirikiana  kusimamia masuala ya udhibiti na usafiri majini.

Makubaliano hayo yalifikiwa visiwani Zanzibar, mwishoni mwa wiki katika kikao cha ushirikiano kilichoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Zanzibar na Wizara ya Uchumi wa Buluu Zanzibar.

Kikao hicho kilichofanyika Ofisi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini, visiwani Zanzibar, kilijadili namna bora ya kuimarisha ushirikiano wa taasisi za usimamizi wa usafiri majini.

Kupitia kikao hicho, taasisi za udhibiti usafiri majini, TASAC chini ya Mkurugenzi Mkuu, Mohamed Salum na ZMA chini ya Mkurugenzi Mkuu, Mtumwa Saidi walijadili changamoto katika usimamizi wa usafiri majini nchini na kuzitafutia ufumbuzi.