TMA yakutana na wadau kuelekea msimu wa Vuli

Na MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imekutana na wadau kutoka sekta mbalimbali nchini kujipanga na Utabiri wa Msimu wa VULI 2024 katika ukumbi wa PSSSF, jijini Dodoma.

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Jaji Mshibe Ali Bakari, aliwahimiza wadau kutoka sekta mbalimbali walioshiriki  mkutano huo kutoa maoni yao sambamba na kutekeleza maazimio ya mkutano yatakayoafikiwa.

” Tunapoelekea kutoa utabiri wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba), 2024 ninawahimiza wadau kutumia jukwaa hili katika kutoa michango ya maoni yenu kikamilifu ili kuleta tija kwa sekta mbalimbali nchini pamoja na kutekeleza maazimio yatakayofikiwa”. Alisema Jaji Mshibe.

 Jaji Mshibe alisisitiza kuwa matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa ni muhimu hususani katika kipindi hiki ambapo dunia pamoja na nchi yetu inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.

“Ninapenda kutoa msisitizo kwenu, katika majadiliano ya mvua za Vuli ya mwaka huu, 2024, mjikite katika kujadili namna ya kuimarisha matumizi ya utabiri wa hali ya hewa mtakaopewa na kushauri hatua stahiki za kuchukua”. Alisisitiza Mhe.Jaji Mshibe.

Akizungumza awali Makamu Mwenyekiti wa Bodi TMA, Dk. Emmanuel Mpeta” ameipongeza TMA kwa kazi nzuri ya kuimarisha ubora na usahihi wa utabiri hususan katika kipindi hiki ambacho Dunia inakabiliwa na mabadiliko ya hali hewa, na kuwaomba wadau wa sekta mbalimbali kuwasilisha maoni yao ya kuimarisha ushauri kwa sekta na jamii.