HOSPITALI YA KAIRUKI YATOA MAFUNZO YA HIFU KWA MADAKTARI BINGWA KUTOKA KENYA

Hospitali ya Kairuki,  imetembelewa na Jumuiya ya Madaktari wa Magonjwa ya wanawake kutoka Kenya (Obstetrical and Gynaecological Society (KOGS), wakiongozwa na Rais wa jumuiya hiyo Dkt. Frederick Kireki.

Ziara hiyo imelenga kufanya  utalii tiba kuboresha huduma za afya Afrika Mashariki na Duniani kwa ujumla, ambapo kupitia ziara hiyo nchini wamepata mafunzo juu ya huduma mpya na ya kisasa iliyotolewa na Hospital ya Kairuki kuondoa uvimbe bila upasuaji kwa kutumia mtambo wa  HIFU na huduma ya Uzazi Pandikizi inayoptolewa na Kairuki Hospital Green IVF.

Akizungumza katika mkutano wa kuwapokea wataalamu hao, Kaimu Mkuu Mkurugenzi wa Hospitali ya Kairuki, Dkt. Muganyizi Kairuki amesisitiza juu ya ushirikiano baina ya pande hizo mbili ikiwemo kufanya utafiti. 

"Ushirikiano wetu udumishe lakini pia tuwe na Tafiti zetu wenyewe juu ya matibabu tofauti tofauti katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki."

Kwa upande wake  Rais wa Jumuiya hiyo Dkt. Frederick Kireki ameishukuru Hospitali ya Kairuki na mapokezi makubwa waliyoyapata  ambapo amesisitiza juu ya kauli mbiu ya “MGONJWA KWANZA” kuwa ni jambo la kujifunza.

Aidha, ugeni huo wa Madaktari wa Magonjwa ya wanawake, ambao upo  Hospitali ya Kairuki kwa muda wa siku mbili, umepata nafasi ya kujionea Mubashara namna ambavyo mtambo wa Kuondoa Uvimbe bila kufanyiwa upasuaji unavyofanya kazi ya kutibu mgonjwa.