Sakata la Kinyesi kutapakaa mtaani la mwibua DC Mpogolo

 Na MWANDISHI WETU

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa wiki mbilli kwa Mamlaka ya  Majisafi na Usafi wa Mazingira  Dar es Salaam (DAWASA) kudhibiti kuvuja kwa kinyesi katika mfumo wa majitaks katika Mtaa wa Kisiwani, Buguruni, jijini  Dar es Salaam.

Aidha, amegiza mamlaka hiyo,  kufumua mfumo huo baada ya kubaini  umejengwa chini ya kiwango.

 Mpogolo  alifika katika eneo hilo kutokana na malalamiko  ya  wananchi kuhusu DAWASA baada ya chemba za mfumo huo kufurika kinyesi  na kuleta adha kubwa.

“Natoa wiki mbili kwa DAWASA , kurekebisha mfumo  huu wa majitaka. Dhamira ya serikali yetu chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kujenga mradi huu siyo kuwaletea  adha wananchi bali ni kuwaondolea kero,”amesema Mpogolo.

Aldha alisema amezungumza na  Mkrugenzi Mtendaji  wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, kufika katika eneo hillo kuukagua mradi  huo na kujiridhisha  juu ya ubora wake.

“Bwire atakuja hapa kesho akague mradi huu  na kujionea hali hii. Pia aangalie ubora wa mradi . Najua ni msikivu na ni mtendaji mzuri,”amesema.

Alisema miongoni mwa changamoto alizobaini  katika mradi huo  ni kujengwa kwa kiwango cha chini, ikiwa ni pamoja na mabomba madogo ya kupitisha maji taka yasiyoendana na wingi wa wakazi wa eneo hilo.

 Mkuu wa Wilaya huyo, alionya vikali wananchi  kutupa taka ngumu katika chemba za mradi huo  hali inayosabababisha kuziba na kuvujisha maji taka.

Ofisa wa DAWASA, Charles Makoye, aliwaomba radhi wananchi wa eneo hilo, huku  akieleza chanzo ni baadhi ya wananchi hao kutupa taka ngumu katika mfumo huo.