JESSICA MSHAMA AUNGA MKONO KAULI YA RAIS SAMIA MSISITIZO WA AMANI NA TIJA YA MAENDLEEO KWA JAMII


Na MWANDISHI WETU

Mjumbe wa Bodi , Baraza la Sanaa Taifa, (BASATA), Balozi Cde. Jessica Mshama, ameunga mkono kauli ya Rais Dk

Samia Suluhu Hassan ya msisitizo wa kulinda amani ikiwa ni msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi.

Pia, alimpongeza Rais Dk.Samia kwa ziara yake anayoendelea kuifanya katika Mkoa wa Ruvuma kukagua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Rais Dk.Samia alitoa kauli hiyo, hivi karibuni katika Tamasha la Tatu la Kitaifa la Utamaduni, lililoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, mkoani Ruvuma, Songea.

Balozi Jessica alisema, kauli hiyo ya Rais Dk.Samia inalenga kudumisha amani na maendeleo ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa jamii na Taifa letu.

"Dhana hizi mbili zina uhusiano wa karibu kwani maendeleo hayawezi kupatikana bila amani na amani inahitajika, kuendeleza ukuaji wa kijamii na kiuchumi. Jamii yenye amani ina uwezekano mkubwa wa kuvutia uwekezaji, kukuza biashara, na kuunda ajira ambazo ni msingi wa maendeleo. Vilevile, maendeleo ya kiuchumi na kijamii inasaidia kuepusha migogoro kwa kupunguza umaskini, ukosefu wa ajira, na kutokuwepo kwa usawa, mambo ambayo mara nyingi ni vyanzo vya migogoro," alisema Mjumbe Jessica.

 Katika hatua nyingine, Mjumbe Jessica  aliwahimiza vijana  kuendeleza juhudi za kujenga na kudumisha amani kwasababu ni muhimu katika kujenga msingi wa maendeleo ya kudumu.