PROFESA KABUDI-TANZANIA ITAENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIHISTORIA NA CHINA

Na MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na China, ambao umekuwa na tija kubwa katika kuleta maendeleo kwa mataifa yote mawili.

Pia, aliishukuru China kwa kuitangaza Tanzania kuwa nchi ya mfano kati ya nchi za Afrika katika ushirikiano  wa karibu wa kidiplomasia na kiuchumi.

Profesa Kabudi ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, katika maadhimisho ya miaka 75 ya watu wa China, yaliyofanyika Ubalozi wa China Nchini na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na mabalozi.

Profesa Kabudi amesema, China na Tanzania ni mataifa rafiki ambapo mahusiano yake yalianzishwa na waasisi wa mataifa hayo akiwemo Mwalimu Julius Nyerere.

"Tangu wakati huo, urafiki huu uliendelea kuimarika awamu kwa awamu hadi awamu hii ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambapo uhusiano huo wa udugu umeimarika zaidi na kuwa na tija kwa Tanzania," amesema.

Amesema Tanzania imeendelea kunufaika na urafiki huo, ambapo mikataba mbalimbali imesainiwa ikiwemo ya kuuza mihogo, pili pili, na wanaenda kuweka makubaliano ya bidhaa za soya nchini china.

Kwa upande wake, Balozi wa  China Nchini, Chen Mingjian amesema furaha yao ni kuona katika maadhimisho ya miaka 70 ya watu wa china, mafanikio makubwa yamefikiwa ya kiuchumi, kibiashara na kidiplomasia.

Amesema katika miaka katika kipindi cha miaka hiyo 75, imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na dunia ikiwemo bara la Afrika ambapo wamekuwa na mikutano mbalimbali ikiwemo ule wa FOCAC, uliofanyika China ambao ulikuwa na tija kubwa ikiwemo mwanzo mpya wa ushirikiano.