Mwenyekiti CCM Tanga aongoza mamia ya wananchi kufanya dua kumwombea Kibao

 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, kikiongozwa na Mwenyekiti wake Rajab Abdallah kushirikiana na uongozi wa Msikiti wa Ijumaa na Familia ya Marehem Ally Mohamed Kibao, wamefanya dua maalumu ya kumrehemu aliyekuwa kiongozi wa Chadema, ambaye alikuwa  mwananchi wa mkoa huo.

Dua hiyo imefanyika leo mkoani Tanga, katika msikiti wa Ijumaa ambapo viongozi mbalimbali waliudhuria wa Chama, serikali na dini kumwombea kiongozi huyo wa kisiasa, ambaye alitekwa na kuuawa na watu wasiojulikana.

Akizungumza baada ya dua hiyo, Mwenyekiti wa CCM Tanga,  Abdallah aliishukuru familia na wanatanga kwa ujumla kukaa kwa utulivu na mshikamano katika kipindi hicho kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao, Kibao, ambaye alizaliwa katika familia ya viongozi wa dini, jambo ambalo limemsukuma kuandaa dua hiyo.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Jafari Kubecha, alimpongeza Mwenyekiti huyo kwa kuandaa dua, huku akiwashukuru  wananchi wa Tanga, kwa subira zao na utulivu wao katika kipindi chote huku akiwataka kuendelea kudumisha umoja na kuungana na familia hiyo.

Awali mwakilishi wa familia, Ally Hemed Abeid alisema familia wanatoa shukrani za dhati kwa jumuiya yote ya watu wa Tanga  akiwemo Mwenyekiti wa CCM Abdallah kwa kuwashika mkono katika kipindi chote hivyo Mwenyezi Mungu atawalipa.