MWENYEKITI WA CCM TANGA, AHIMIZA WANANCHI KUMWOMBEA RAIS SAMIA KWA KAZI KUBWA ANAYOIFANYA



MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah, amehimiza wananchi wa Tanga na Tanzania kwa ujumla kumwombea Rais Dk.Samia kwa kazi kubwa anayoifanya.

Mwenyekiti Abdallah ameyasema hayo mkoani humo, katika msikiti wa Ijumaa, uliopo Wilaya ya Tanga Mjini, baada ya dua ya kumrehemu aliyekuwa kiongozi wa Chadema Marehem Ally Mohamed Kibao aliyetekwa na kuuawa na watu wasio julikana hivi karibuni.

"Tuendelee kumwombea Rais Dk.Samia kwa kazi kubwa anayoifanya, kuongoza nchi sio mchezo ni jambo kubwa, Tuendelea kumwombea Rais Dk.Samia katika uongozi wake kwa jukumu kubwa alilonalo la kuongoza nchi,"amesisitiza.

Vilevile, aliwapongeza wanafamilia ya marehemu  Ali Kibao, kwa utulivu na ushirikiano wao kwa kukubali kufanyika dua hiyo huku akiwashukuru wananchi wa Tanga kwa kujitokeza kwa wingi katika Dua hiyo kuunga kuwafariji wanafamilia.

Awali mwakilishi wa familia ya Ali Kibao, Ally Hemed Abeid amesema familia wanatoa shukrani za dhati kwa jumuiya yote ya watu wa Tanga  akiwemo Mwenyekiti wa CCM Abdallah kwa kuwashika mkono katika kipindi chote hivyo Mwenyezi Mungu atawalipa.