MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama, amempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kauli yake dhabiti ya kukemea utekaji, ukuaji na kuagiza Mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina kubaini waliohusika na mauaji ya Ally Mohamed Kibao.
Rajab ameyasema hayo, mkoani Tanga katika Msikiti wa Ijumaa, baada ya dua maalumu aliyoiandaa kushirikiana na vingozi wa dini wa mkoa huo, kwaajili ya Kibao huku mamia ya wananchi na viongozi wa Chama na serikali wakiudhuria.
"Katika hili, tumesikia kauli ya Rais Dk.Samia ya kusikitishwa na tukio hili, kukemea katika hili na matukio mengine yanayo shabihiana na hili, Tunampongeza Rais Dk.Samia kwa kauli yake ya kukemea vitendo hivyo viovu, ambavyo havipendezi, tunaunga mkono kauli yake ya kutoa maelekezo kwa Mamlaka husika, kuhakikisha uchunguzi wa kina na weledi, kuhakikisha vikundi na wote waliohusika na vitendo hivi wanakamatwa," amesema.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Jafari Kubecha, aliwashukuru wananchi wa Tanga, kwa subira zao na utulivu wao katika kipindi chote huku akiwataka kuendelea kudumisha umoja na kuungana na familia hiyo.
Alisema, Mkoa na Wilaya hiyo ni salama na wataendelea kudumisha umoja na usalama na hawataruhusu mtu yeyote kuvuruga amani iliyopo ambapo serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali za dini kuhudumia wananchi.